1.

Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba,

2.

Amemuumba binaadamu kwa tone la damu,

3.

Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote!

4.

Ambaye amefundisha kwa kalamu.

5.

Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui.

6.

Kwani! Hakika mtu bila ya shaka huwa jeuri

7.

Akijiona katajirika.

8.

Hakika kwa Mola wako Mlezi ndio marejeo.

9.

Umemwona yule anaye mkataza

10.

Mja anapo sali?

11.

Umeona kama yeye yuko juu ya uwongofu?

12.

Au anaamrisha uchamngu?

13.

Umeona kama yeye akikanusha na anarudi nyuma?

14.

Hajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anaona?

15.

Kwani! Kama haachi, tutamkokota kwa shungi la nywele!

16.

Shungi la uwongo, lenye makosa!

17.

Basi na awaite wenzake!

18.

Nasi tutawaita Mazabania!

19.

Hasha! Usimt’ii! Nawe sujudu na ujongee!