1. |
Naapa kwa jua na mwangaza wake! |
2. |
Na kwa mwezi unapo lifuatia! |
3. |
Na kwa mchana unapo lidhihirisha! |
4. |
Na kwa usiku unapo lifunika! |
5. |
Na kwa mbingu na kwa aliye ijenga! |
6. |
Na kwa ardhi na kwa aliye itandaza! |
7. |
Na kwa nafsi na kwa aliye itengeneza! |
8. |
Kisha akaifahamisha uovu wake na wema wake, |
9. |
Hakika amefanikiwa aliye itakasa, |
10. |
Na hakika amekhasiri aliye iviza. |
11. |
Kina Thamudi walikadhibisha kwa sababu ya upotofu wao, |
12. |
Alipo simama mwovu wao mkubwa, |
13. |
Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu alipo waambia: Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu, mwacheni anywe maji fungu lake. |
14. |
Lakini walimkadhibisha na wakamchinja ngamia, kwa hivyo Mola wao Mlezi aliwaangamiza kwa sababu ya dhambi zao na akawafuta kabisa. |
15. |
Wala Yeye haogopi matokeo yake. |