1.

Naapa kwa alfajiri,

2.

Na kwa masiku kumi,

3.

Na kwa viwili viwili na kimoja kimoja,

4.

Na kwa usiku unapo pita,

5.

Je! Hapana katika haya kiapo kwa mwenye akili?

6.

Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo wafanya kina A’di?

7.

Wa Iram, wenye majumba marefu?

8.

Ambao haukuumbwa mfano wake katika nchi?

9.

Na Thamudi walio chonga majabali huko bondeni?

10.

Na Firauni mwenye vigingi?

11.

Ambao walifanya jeuri katika nchi?

12.

Wakakithirisha humo ufisadi?

13.

Basi Mola wako Mlezi aliwapiga mjeledi wa adhabu.

14.

Hakika Mola wako Mlezi yupo kwenye mavizio anawavizia.

15.

Ama mtu anapo jaribiwa na Mola wake Mlezi, akamkirimu na akamneemesha, husema: Mola wangu Mlezi amenikirimu!

16.

Na ama anapo mjaribu akampunguzia riziki yake, husema: Mola wangu Mlezi amenitia unyonge!

17.

Sivyo hivyo! Bali nyinyi hamuwakirimu mayatima,

18.

Wala hamhimizani kulisha masikini;

19.

Na mnakula urithi kwa ulaji wa pupa,

20.

Na mnapenda mali pendo la kupita kiasi.

21.

Sivyo hivyo! Itakapo vunjwa ardhi vipande vipande,

22.

Na akaja Mola wako Mlezi na Malaika safu safu,

23.

Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini?

24.

Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu!

25.

Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake.

26.

Wala hatafunga yeyote kama kufunga kwake.

27.

Ewe nafsi iliyo tua!

28.

Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha.

29.

Basi ingia miongoni mwa waja wangu,

30.

Na ingia katika Pepo yangu.