1. |
Je! Imekufikia khabari ya msiba wa kufudikiza? |
2. |
Siku hiyo nyuso zitainama, |
3. |
Zikifanya kazi, nazo taabani. |
4. |
Ziingie katika Moto unao waka – |
5. |
Zikinyweshwa kutoka chemchem inayo chemka. |
6. |
Hawatakuwa na chakula isipo kuwa kichungu chenye miba. |
7. |
Hakinenepeshi wala hakiondoi njaa. |
8. |
Siku hiyo nyuso nyengine zitakuwa kunjufu. |
9. |
Zitakuwa radhi kwa juhudi yao, |
10. |
Katika Bustani ya juu. |
11. |
Hawatasikia humo upuuzi. |
12. |
Humo imo chemchem inayo miminika. |
13. |
Humo vimo viti vilivyo nyanyuliwa, |
14. |
Na bilauri zilizo pangwa, |
15. |
Na matakia safu safu, |
16. |
Na mazulia yaliyo tandikwa. |
17. |
Je! Hawamtazami ngamia jinsi alivyo umbwa? |
18. |
Na mbingu jinsi ilivyo inuliwa? |
19. |
Na milima jinsi ilivyo thibitishwa? |
20. |
Na ardhi jinsi ilivyo tandazwa? |
21. |
Basi kumbusha! Hakika wewe ni Mkumbushaji. |
22. |
Wewe si mwenye kuwatawalia. |
23. |
Lakini anaye rudi nyuma na kukataa, |
24. |
Basi Mwenyezi Mungu atamuadhibu kwa adhabu iliyo kubwa kabisa! |
25. |
Hakika ni kwetu Sisi ndio marejeo yao. |
26. |
Kisha hakika ni juu yetu Sisi hisabu yao! |