1. |
Naapa kwa mbingu yenye Buruji! |
2. |
Na kwa siku iliyo ahidiwa! |
3. |
Na kwa shahidi na kinacho shuhudiwa! |
4. |
Wameangamizwa watu wa makhandaki |
5. |
Yenye moto wenye kuni nyingi, |
6. |
Walipo kuwa wamekaa hapo, |
7. |
Na wao ni mashahidi wa yale waliyo kuwa wakiwafanyia Waumini. |
8. |
Nao hawakuona baya lolote kwao ila kuwa wakimuamini Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Msifiwa, |
9. |
Ambaye anao ufalme wa mbingu na ardhi; na Mwenyezi Mungu ni shaahidi wa kila kitu. |
10. |
Hakika walio wafitini Waumini wanaume na Waumini wanawake, kisha hawakutubu, basi watapata adhabu ya Jahannamu na watapata adhabu ya kuungua. |
11. |
Hakika walio amini na wakatenda mema watapata Bustani zenye mito ipitayo kati yake. Huko ndiko kufuzu kukubwa. |
12. |
Hakika kutesa kwa Mola wako Mlezi ni kukali. |
13. |
Yeye ndiye anaye anzisha na ndiye anaye rejeza tena, |
14. |
Naye ni Mwenye kusamehe, Mwenye mapenzi, |
15. |
Mwenye Kiti cha Enzi, Mtukufu, |
16. |
Atendaye ayatakayo. |
17. |
Je! Zimekuwasilia khabari za majeshi? |
18. |
Ya Firauni na Thamudi? |
19. |
Lakini walio kufuru wamo katika kukadhibisha. |
20. |
Na Mwenyezi Mungu nyuma yao amewazunguka. |
21. |
Bali hii ni Qur’ani tukufu |
22. |
Katika Ubao Ulio Hifadhiwa. |