1.

Ole wao hao wapunjao!

2.

Ambao wanapo jipimia kwa watu hudai watimiziwe.

3.

Na wao wanapo wapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza.

4.

Kwani hawadhani hao kwamba watafufuliwa

5.

Katika Siku iliyo kuu,

6.

Siku watapo msimamia watu Mola Mlezi wa walimwengu wote?

7.

Hasha! Hakika maandiko ya wakosefu bila ya shaka yamo katika Sijjin.

8.

Unajua nini Sijjin?

9.

Kitabu kilicho andikwa.

10.

Ole wao siku hiyo kwa wanao kadhibisha!

11.

Ambao wanaikadhibisha Siku ya Malipo.

12.

Wala haikadhibishi ila kila mwenye kuruka mipaka, mwenye dhambi.

13.

Anapo somewa Aya zetu husema: Ni visa vya watu wa kale!

14.

Hasha! Bali yametia kutu juu ya nyoyo zao hao walio kuwa wakiyachuma.

15.

Hasha! Hakika hao siku hiyo bila ya shaka watazuiliwa na neema za Mola wao Mlezi.

16.

Kisha wataingia Motoni!

17.

Kisha waambiwe: Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyakadhabisha.

18.

Hasha! Hakika maandiko ya watu wema bila ya shaka yamo katika I’liyyin.

19.

Na nini kitakacho kujuvya nini I’liyyin?

20.

Kitabu kilicho andikwa.

21.

Wanakishuhudia walio karibishwa.

22.

Hakika watu wema bila ya shaka watakuwa katika neema.

23.

Wakae juu ya viti vya enzi wakiangalia.

24.

Utatambua katika nyuso zao mng’aro wa neema,

25.

Watanyweshwa kinywaji safi kiliyo tiwa muhuri,

26.

Muhuri wake ni miski. Na katika hayo washindanie wenye kushindana.

27.

Na mchanganyiko wake ni Tasniim,

28.

Chemchem watakayo inywa walio kurubishwa.

29.

Kwa hakika wale walio kuwa wakosefu walikuwa wakiwacheka walio amini.

30.

Na wanapo pita karibu yao wakikonyezana.

31.

Na wanapo rudi kwa watu wao hurudi nao wamefurahi.

32.

Na wanapo waona husema: Hakika hawa ndio khasa walio potea.

33.

Na wao hawakutumwa wawe walinzi juu yao.

34.

Basi leo walio amini ndio watawacheka makafiri,

35.

Nao wako juu ya viti vya enzi wakiangalia.

36.

Je! makafiri wamelipwa malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda?