80. A’basa

1.

Alikunja kipaji na akageuka,

2.

Kwa sababu alimjia kipofu!

3.

Na nini kitakujuulisha pengine yeye atatakasika?

4.

Au atawaidhika, na mawaidha yamfae?

5.

Ama ajionaye hana haja,

6.

Wewe ndio unamshughulikia?

7.

Na si juu yako kama hakutakasika.

8.

Ama anaye kujia kwa juhudi,

9.

Naye anaogopa,

10.

Ndio wewe unampuuza?

11.

Sivyo hivyo! Huku ni kukumbushana.

12.

Basi anaye penda akumbuke.

13.

Yamo katika kurasa zilizo hishimiwa,

14.

Zilizo inuliwa, zilizo takaswa.

15.

Zimo mikononi mwa Malaika waandishi,

16.

Watukufu, wema.

17.

Ameangamia mwanaadamu! Nini kinacho mkufurisha?

18.

Kwa kitu gani amemuumba?

19.

Kwa tone la manii, akamuumba na akamkadiria.

20.

Kisha akamsahilishia njia.

21.

Kisha akamfisha, akamtia kaburini.

22.

Kisha apendapo atamfufua.

23.

La! Hajamaliza aliyo muamuru.

24.

Hebu mtu na atazame chakula chake.

25.

Hakika Sisi tumemimina maji kwa nguvu,

26.

Tena tukaipasua pasua ardhi kwa nguvu,

27.

Kisha tukaotesha humo nafaka,

28.

Na zabibu, na mimea ya majani,

29.

Na mizaituni, na mitende,

30.

Na bustani zenye miti iliyo songana baraabara,

31.

Na matunda, na malisho ya wanyama;

32.

Kwa manufaa yenu na mifugo yenu.

33.

Basi utakapo kuja ukelele,

34.

Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye,

35.

Na mamaye na babaye,

36.

Na mkewe na wanawe –

37.

Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha.

38.

Siku hiyo ziko nyuso zitazo nawiri,

39.

Zitacheka, zitachangamka;

40.

Na nyuso siku hiyo zitakuwa na mavumbi,

41.

Giza totoro litazifunika,

42.

Hao ndio makafiri watenda maovu.