1.

Naapa kwa wanao komoa kwa nguvu,

2.

Na kwa wanao toa kwa upole,

3.

Na wanao ogelea,

4.

Wakishindana mbio,

5.

Wakidabiri mambo.

6.

Siku kitapo tetemeka cha kutetemeka,

7.

Kifuate cha kufuatia.

8.

Siku hiyo nyoyo zitapiga piga,

9.

Macho yatainama chini.

10.

Sasa wanasema: Ati kweli tutarudishwa kwenye hali ya kwanza?

11.

Hata tukiwa mifupa iliyo bunguliwa?

12.

Wanasema: Basi marejeo hayo ni yenye khasara!

13.

Kwa hakika hayo ni ukelele mmoja tu,

14.

Mara watakuwa kwenye uwanda wa mkutano!

15.

Je! Imekufikia hadithi ya Musa?

16.

Mola wake Mlezi alipo mwita katika bonde takatifu la T’uwaa, akamwambia:

17.

Nenda kwa Firauni. Hakika yeye amezidi jeuri.

18.

Umwambie: Je! Unapenda kujitakasa?

19.

Nami nitakuongoa ufike kwa Mola wako Mlezi, upate kumcha.

20.

Basi alimwonyesha Ishara kubwa.

21.

Lakini aliikadhibisha na akaasi.

22.

Kisha alirudi nyuma, akaingia kufanya juhudi.

23.

Akakusanya watu akanadi.

24.

Akasema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi mkuu kabisa.

25.

Basi hapo Mwenyezi Mungu akamshika kumuadhibu kwa la mwisho na la mwanzo.

26.

Kwa hakika katika haya yapo mazingatio kwa wanao ogopa.

27.

Je! Ni vigumu zaidi kukuumbeni nyinyi au mbingu? Yeye ndiye aliye ijenga!

28.

Akainua kimo chake, na akaitengeneza vizuri.

29.

Na akautia giza usiku wake, na akautokeza mchana wake.

30.

Na juu ya hivyo ameitandaza ardhi.

31.

Akatoa ndani yake maji yake na malisho yake,

32.

Na milima akaisimamisha,

33.

Kwa nafuu yenu na mifugo yenu.

34.

Basi itakapo fika hiyo balaa kubwa,

35.

Siku ambayo mtu atakumbuka aliyo yafanya,

36.

Na Jahannamu itadhihirishwa kwa mwenye kuona,

37.

Basi ama yule aliye zidi ujeuri,

38.

Na akakhiari maisha ya dunia,

39.

Kwa hakika Jahannamu ndiyo makaazi yake!

40.

Na ama yule anaye ogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuilia nafsi yake na matamanio,

41.

Basi huyo, Pepo itakuwa ndiyo makaazi yake!

42.

Wanakuuliza Saa (ya Kiyama) itakuwa lini?

43.

Una nini wewe hata uitaje?

44.

Kwa Mola wako Mlezi ndio mwisho wake.

45.

Kwa hakika wewe ni mwonyaji tu kwa mwenye kuikhofu.

46.

Ni kama kwamba wao siku watapo iona (hiyo Saa) hawakukaa ila jioni moja tu, au mchana wake.