1. |
WANAULIZANA nini? |
2. |
Ile khabari kuu, |
3. |
Ambayo kwayo wanakhitalifiana. |
4. |
La! Karibu watakuja jua. |
5. |
Tena la! Karibu watakuja jua. |
6. |
Kwani hatukuifanya ardhi kama tandiko? |
7. |
Na milima kama vigingi? |
8. |
Na tukakuumbeni kwa jozi? |
9. |
Na tukakufanya kulala kwenu ni mapumziko? |
10. |
Na tukaufanya usiku ni nguo? |
11. |
Na tukaufanya mchana ni wa kuchumia maisha? |
12. |
Na tukajenga juu yenu saba zenye nguvu? |
13. |
Na tukaifanya taa yenye mwanga na joto; |
14. |
Na tukateremsha maji yanayo anguka kwa kasi kutoka mawinguni, |
15. |
Ili tutoe kwayo nafaka na mimea, |
16. |
Na mabustani yenye miti iliyo kamatana. |
17. |
Hakika siku ya uamuzi imewekewa wakati wake, |
18. |
Siku litapo pulizwa barugumu, nanyi mtakuja kwa makundi, |
19. |
Na mbingu zitafunguliwa, ziwe milango, |
20. |
Na milima itaondolewa na itakuwa kama sarabi. |
21. |
Hakika Jahannamu inangojea! |
22. |
Kwa walio asi ndio makaazi yao, |
23. |
Wakae humo karne baada ya karne, |
24. |
Hawataonja humo chochote kibaridi wala kinywaji, |
25. |
Ila maji yamoto sana na usaha, |
26. |
Ndio jaza muwafaka. |
27. |
Hakika hao hawakuwa wakitaraji kuwa kuna hisabu. |
28. |
Na wakikanusha Aya zetu kwa nguvu. |
29. |
Na kila kitu Sisi tumekidhibiti kwa kukiandika. |
30. |
Basi onjeni! Nasi hatutakuzidishieni ila adhabu! |
31. |
Hakika wachamngu wanastahiki kufuzu, |
32. |
Mabustani na mizabibu, |
33. |
Na wake walio lingana nao, |
34. |
Na bilauri zilizo jaa, |
35. |
Hawatasikia humo upuuzi wala uwongo – |
36. |
Malipo kutoka kwa Mola wako Mlezi, kipawa cha kutosha. |
37. |
Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, Arrahman, Mwingi wa rehema; hawamiliki usemi mbele yake! |
38. |
Siku atakapo simama Roho na Malaika kwa safu. Hawatasema ila Mwingi wa rehema aliye mruhusu, na atasema yaliyo sawa tu. |
39. |
Hiyo ndiyo Siku ya haki. Basi anaye taka na ashike njia arejee kwa Mola wake Mlezi. |
40. |
Hakika tumekuhadharisheni adhabu iliyo karibu kufika; Siku ambayo mtu atakapo ona yaliyo tangulizwa na mikono yake; na kafiri atasema: Laiti ningeli kuwa udongo! |