1. |
Hakika kilimpitia binaadamu kipindi katika zama ambacho kwamba hakuwa kitu kinacho tajwa. |
2. |
Hakika Sisi tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyo changanyika, tumfanyie mtihani. Kwa hivyo tukamfanya mwenye kusikia, mwenye kuona. |
3. |
Hakika Sisi tumembainishia Njia. Ama ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru. |
4. |
Hakika Sisi tumewaandalia makafiri minyororo na pingu na Moto mkali. |
5. |
Hakika watu wema watakunywa katika vinywaji vilivyo changanyika na kafuri, |
6. |
Ni chemchem watakao inywa waja wa Mwenyezi Mungu, wakiifanya imiminike kwa wingi. |
7. |
Wanatimiza ahadi, na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana, |
8. |
Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa. |
9. |
Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani. |
10. |
Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu Mlezi hiyo siku yenye shida na taabu. |
11. |
Basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na raha na furaha. |
12. |
Na atawajazi Bustani za Peponi na maguo ya hariri kwa vile walivyo subiri. |
13. |
Humo wataegemea juu ya viti vya enzi, hawataona humo jua kali wala baridi kali. |
14. |
Na vivuli vyake vitakuwa karibu yao, na mashada ya matunda yataning’inia mpaka chini. |
15. |
Na watapitishiwa vyombo vya fedha na vikombe vya vigae, |
16. |
Vya fedha safi kama kiyoo, wamevipima kwa vipimo. |
17. |
Na humo watanyweshwa kinywaji kilicho changanyika na tangawizi. |
18. |
Hiyo ni chemchem iliyo humo inaitwa Salsabil. |
19. |
Na watawazungukia kuwatumikia wavulana wasio pevuka, ukiwaona utawafikiri ni lulu zilizo tawanywa. |
20. |
Na utakapo yaona, utakuwa umeona neema na ufalme mkubwa. |
21. |
Juu yao zipo nguo za hariri laini za kijani kibichi, na hariri nzito ya at’ilasi. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao Mlezi atawanywesha kinywaji safi kabisa. |
22. |
Hakika haya ni malipo yenu; na juhudi zenu zimekubaliwa. |
23. |
Hakika Sisi tumekuteremshia Qur’ani kidogo kidogo. |
24. |
Basi ngojea hukumu ya Mola wako Mlezi wala usimt’ii miongoni mwao mwenye dhambi au mwenye kufuru. |
25. |
Na likumbuke jina la Mola wako Mlezi asubuhi na jioni; |
26. |
Na usiku msujudie Yeye, na umtakase usiku, wakati mrefu. |
27. |
Kwa hakika watu hawa wanapenda maisha ya kidunia, na wanaiacha nyuma yao siku nzito. |
28. |
Sisi tumewaumba, na tukavitia nguvu viungo vyao. Na tukitaka tutawabadilisha mfano wao wawe badala yao. |
29. |
Hakika haya ni mawaidha; basi anaye taka atashika Njia ya kwenda kwa Mola wake Mlezi. |
30. |
Wala hamwezi kutaka ila atakapo Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ilimu, Mwenye hikima. |
31. |
Humuingiza amtakaye katika rehema yake. Na wenye kudhulumu amewawekea adhabu iliyo chungu. |