75. Al-Qiyamah

1.

Ninaapa kwa Siku ya Kiyama!

2.

Na ninaapa kwa nafsi inayo jilaumu!

3.

Anadhani mtu kuwa Sisi hatutaikusanya mifupa yake?

4.

Kwani! Sisi tunaweza hata kuziweka sawa sawa ncha za vidole vyake!

5.

Lakini mtu anataka tu kuendelea na maasi kwa siku zilioko mbele yake.

6.

Anauliza: Lini itakuwa hiyo Siku ya Kiyama?

7.

Basi jicho litapo dawaa,

8.

Na mwezi utapo patwa,

9.

Na likakusanywa jua na mwezi,

10.

Siku hiyo mtu atasema: Yako wapi makimbilio?

11.

La! Hapana pa kukimbilia!

12.

Siku hiyo pa kutua ni kwa Mola wako Mlezi tu.

13.

Siku hiyo ataambiwa aliyo yatanguliza na aliyo yaakhirisha.

14.

Bali mtu ni hoja juu ya nafsi yake.

15.

Na ingawa atatoa chungu ya udhuru.

16.

Usiutikisie huu wahyi ulimi wako kwa kuufanyia haraka.

17.

Hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha.

18.

Tunapo usoma, basi nawe fuatiliza kusoma kwake.

19.

Kisha ni juu yetu kuubainisha.

20.

Hasha! Bali nyinyi mnapenda maisha ya duniani,

21.

Na mnaacha maisha ya Akhera.

22.

Zipo nyuso siku hiyo zitao ng’ara,

23.

Zinamwangallia Mola wao Mlezi.

24.

Na zipo nyuso siku hiyo zitakao kunjana.

25.

Zitajua ya kuwa zitafikiwa na livunjalo uti wa mgongo.

26.

La, hasha! (Roho) itakapo fikia kwenye mafupa ya koo,

27.

Na pakasemwa: Nani wa kumganga?

28.

Na mwenyewe akajua kwa hakika kuwa huko ndiko kufariki;

29.

Na utapo ambatishwa muundi kwa muundi,

30.

Siku hiyo ndiyo kuchungwa kupelekwa kwa Mola wako Mlezi!

31.

Kwa sababu hakusadiki, wala hakusali.

32.

Bali alikanusha, na akageuka.

33.

Kisha akenda kwa ahali zake kwa matao.

34.

Ole wako, ole wako!

35.

Kisha Ole wako, ole wako!

36.

Ati anadhani binaadamu kuwa ataachwa bure?

37.

Kwani hakuwa yeye tone ya manii lilio shushwa?

38.

Kisha akawa kidonge cha damu, tena Mwenyezi Mungu akamuumba na akamtengeneza vilivyo.

39.

Kisha akamfanya namna mbili, mwanamume na mwanamke.

40.

Je! Huyo hakuwa ni Muweza wa kufufua wafu?