1.

Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayo tokea,

2.

Kwa makafiri – ambayo hapana awezaye kuizuia –

3.

Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu za daraja.

4.

Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka khamsini elfu!

5.

Basi subiri kwa subira njema.

6.

Hakika wao wanaiona iko mbali,

7.

Na Sisi tunaiona iko karibu.

8.

Siku ambayo mbingu zitakapo kuwa kama maadeni iliyo yayushwa.

9.

Na milima itakuwa kama sufi.

10.

Wala jamaa hatamuuliza jamaa yake.

11.

Ijapo kuwa wataonyeshwa waonane. Atatamani mkosefu lau ajikomboe na adhabu ya siku hiyo kwa kuwatoa fidia wanawe,

12.

Na mkewe, na nduguye,

13.

Na jamaa zake walio kuwa wakimkimu,

14.

Na wote waliomo duniani, kisha aokoke yeye.

15.

La, hasha! Kwa hakika huo ni Moto mkali kabisa,

16.

Unao babua ngozi ya kichwa!

17.

Utamwita kila aliye geuza mgongo na akageuka.

18.

Na akakusanya mali, kisha akayahifadhi.

19.

Hakika mtu ameumbwa na papara.

20.

Inapo mgusa shari hupapatika.

21.

Na inapo mgusa kheri huizuilia.

22.

Isipo kuwa wanao sali,

23.

Ambao wanadumisha Sala zao,

24.

Na ambao katika mali yao iko haki maalumu

25.

Kwa mwenye kuomba na anaye jizuilia kuomba;

26.

Na ambao wanaisadiki Siku ya Malipo,

27.

Na ambao wanaiogopa adhabu itokayo kwa Mola wao Mlezi.

28.

Hakika adhabu ya Mola wao Mlezi si ya kuaminika nayo.

29.

Na ambao wanahifadhi tupu zao.

30.

Isipo kuwa kwa wake zao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, basi hao hawalaumiwi –

31.

Lakini wanao taka kinyume ya haya, basi hao ndio wanao ruka mipaka.

32.

Na ambao wanazichunga amana zao na ahadi zao,

33.

Na ambao wanasimama imara katika ushahidi wao,

34.

Na ambao wanazihifadhi Sala zao.

35.

Hao ndio watakao hishimiwa Peponi.

36.

Wana nini wale walio kufuru wanakutumbulia macho tu?

37.

Makundi kwa makundi upande wa kulia na upande wa kushoto!

38.

Kwani kila mmoja wao anatumai kuingizwa katika Pepo ya neema?

39.

La, hasha! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na wanacho kijua.

40.

Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mashariki zote na magharibi zote kwamba Sisi tunaweza

41.

Kuwabadili kwa walio bora kuliko wao; na Sisi hatushindwi.

42.

Basi waache wapige porojo na wacheze, mpaka wakutane na siku yao wanayo ahidiwa,

43.

Siku watakapotoka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia mfundo,

44.

Macho yao yatainama, fedheha itawafunika. Hiyo ndiyo Siku waliyo kuwa wakiahidiwa.