1. |
Tukio la haki. |
2. |
Nini hilo Tukio la haki? |
3. |
Na nini kitakujuulisha nini hilo Tukio la haki? |
4. |
Thamudi na A’di waliukadhibisha Msiba unao situsha. |
5. |
Basi Thamudi waliangamizwa kwa balaa kubwa mno. |
6. |
Na ama A’di waliangamizwa kwa upepo mkali usio zuilika. |
7. |
Alio wapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo bila ya kusita. Utaona watu wamepinduka kama kwamba ni magongo ya mitende yalio wazi ndani. |
8. |
Basi je! Unamwona mmoja wao aliye baki? |
9. |
Na Firauni na walio mtangulia, na miji iliyo pinduliwa chini juu, walileta khatia. |
10. |
Wakamuasi Mtume wa Mola wao Mlezi, ndipo Yeye Mola akawakamata kwa mkamato ulio zidi nguvu. |
11. |
Maji yalipo furika Sisi tulikupandisheni katika safina, |
12. |
Ili tuyafanye hayo kuwa ni waadhi kwenu na kila sikio linalo sikia liyahifadhi. |
13. |
Na litapo pulizwa barugumu mpulizo mmoja tu, |
14. |
Na ardhi na milima ikaondolewa, na ikavunjwa kwa mvunjo mmoja, |
15. |
Siku hiyo ndio Tukio litatukia. |
16. |
Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa. |
17. |
Na Malaika watakuwa pembezoni mwa mbingu; na wanane juu ya hawa watakuwa wamebeba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi. |
18. |
Siku hiyo mtahudhurishwa – haitafichika siri yoyote yenu. |
19. |
Basi ama atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu! |
20. |
Hakika nalijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu. |
21. |
Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza, |
22. |
Katika Bustani ya juu, |
23. |
Matunda yake yakaribu. |
24. |
Waambiwe: Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya mlivyo tanguliza katika siku zilizo pita. |
25. |
Na ama atakaye pewa kitabu chake katika mkono wake wa kushoto, basi yeye atasema: Laiti nisingeli pewa kitabu changu! |
26. |
Wala nisingeli jua nini hisabu yangu. |
27. |
Laiti mauti ndiyo yangeli kuwa ya kunimaliza kabisa. |
28. |
Mali yangu hayakunifaa kitu. |
29. |
Madaraka yangu yamenipotea. |
30. |
(Pasemwe): Mshikeni! Mtieni pingu! |
31. |
Kisha mtupeni Motoni! |
32. |
Tena mtatizeni katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabiini! |
33. |
Kwani huyo hakika alikuwa hamuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, |
34. |
Wala hahimizi kulisha masikini. |
35. |
Basi leo hapa hana jamaa wa kumwonea uchungu, |
36. |
Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni. |
37. |
Chakula hicho hawakili ila wakosefu. |
38. |
Basi naapa kwa mnavyo viona, |
39. |
Na msivyo viona, |
40. |
Kwa hakika hii ni kauli iliyo letwa na Mjumbe mwenye hishima. |
41. |
Wala si kauli ya mtunga mashairi. Ni machache sana mnayo yaamini. |
42. |
Wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayo yakumbuka. |
43. |
Ni uteremsho utokao kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. |
44. |
Na lau kama angeli tuzulia baadhi ya maneno tu, |
45. |
Bila ya shaka tungeli mshika kwa mkono wa kulia, |
46. |
Kisha kwa hakika tungeli mkata mshipa mkubwa wa moyo! |
47. |
Na hapana yeyote katika nyinyi ambaye angeli weza kutuzuia. |
48. |
Kwa hakika hii ni mawaidha kwa wachamngu. |
49. |
Na hakika Sisi bila ya shaka tunajua kwamba miongoni mwenu wapo wanao kadhibisha. |
50. |
Na hakika bila ya shaka itakuwa ni majuto kwa wanao kataa. |
51. |
Na hakika hii bila ya shaka ni haki ya yakini. |
52. |
Basi litakase jina la Mola wako Mlezi Mtukufu. |