1. |
AMETUKUKA ambaye mkononi mwake umo Ufalme wote; na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. |
2. |
Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha. |
3. |
Aliye umba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudisha nadhari! Unaona kosa lolote? |
4. |
Tena rudisha nadhari mara mbili, nadhari yako itakurejea mwenyewe hali ya kuwa imehizika nayo imechoka. |
5. |
Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa, na tumeyafanya ili kuwapigia mashetani, na tumewaandalia adhabu ya Moto uwakao kwa nguvu. |
6. |
Na kwa walio mkufuru Mola wao Mlezi ipo adhabu ya Jahannamu. Na ni marejeo maovu yalioje hayo! |
7. |
Watakapo tupwa humo watausikia mngurumo wake na huku inafoka. |
8. |
Inakaribia kupasuka kwa hasira. Kila mara likitupwa kundi humo walinzi wake huwauliza: Kwani hakukujieni mwonyaji? |
9. |
Watasema: Kwani! Ametujia mwonyaji, lakini tulimkadhibisha, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote. Nyinyi hamumo ila katika upotovu mkubwa! |
10. |
Na watasema: Lau kuwa tungeli sikia, au tungeli kuwa na akili, tusingeli kuwa katika watu wa Motoni! |
11. |
Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa Motoni! |
12. |
Hakika wanao mwogopa Mola wao Mlezi kwa ghaibu, watapata maghfira na ujira mkubwa. |
13. |
Na ficheni kauli zenu, au zitangazeni; hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani. |
14. |
Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari? |
15. |
Yeye ndiye aliye idhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. Na kwake Yeye ndio kufufuliwa. |
16. |
Mnadhani mko salama kwa alioko juu kuwa hatakudidimizeni kwenye ardhi, na tahamaki hiyo inatikisika! |
17. |
Au mnadhani mko salama kwa alioko juu ya kuwa Yeye hakupelekeeni kimbunga chenye changarawe? Mtajua vipi maonyo yangu? |
18. |
Na bila ya shaka walikwisha kanusha walio kuwa kabla yao; basi kulikuwaje kukasirika kwangu? |
19. |
Kwani hawawaoni ndege walioko juu yao namna wanavyo zikunjua mbawa zao, na kuzikunja? Hawawashikilii ila Mwingi wa rehema. Hakika Yeye ni Mwenye kuona kila kitu. |
20. |
Au ni lipi hilo jeshi lenu la kukunusuruni badala ya Mwingi wa Rehema? Hakika makafiri hawamo ila katika udanganyifu. |
21. |
Au ni nani huyo ambaye atakupeni riziki kama Yeye akizuia riziki yake? Bali wao wanakakamia tu katika jeuri na chuki. |
22. |
Je! Anaye kwenda akisinukia juu ya uso wake ni mwongofu zaidi, au yule anaye kwenda sawasawa katika Njia Iliyo Nyooka? |
23. |
Sema: Yeye ndiye aliye kuumbeni tangu mwanzo, na akakupeni masikio na macho, na nyoyo. Ni kidogo kabisa shukrani zenu. |
24. |
Sema: Yeye ndiye aliye kutawanyeni katika ardhi, na kwake mtakusanywa. |
25. |
Na wanasema: Lini ahadi hii, ikiwa mnasema kweli? |
26. |
Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu; na hakika mimi ni mwonyaji tu mwenye kubainisha. |
27. |
Lakini watakapo iona karibu, nyuso za walio kufuru zitahuzunishwa, na itasemwa: Hayo ndiyo mliyo kuwa mkiyaomba. |
28. |
Sema: Mwaonaje, ikiwa Mwenyezi Mungu atanihiliki mimi na walio pamoja nami, au akiturehemu, ni nani atakaye walinda makafiri na adhabu chungu? |
29. |
Sema: Yeye ndiye Mwingi wa Rehema; tunamuamini Yeye, na juu yake tunategemea. Mtakuja jua ni nani aliye katika upotovu ulio dhaahiri. |
30. |
Sema: Mwaonaje, yakiwa maji yenu yamedidimia chini, nani atakueleteeni maji yanayo miminika? |