1. |
Litakapo tukia hilo Tukio |
2. |
Hapana cha kukanusha kutukia kwake. |
3. |
Literemshalo linyanyualo, |
4. |
Itakapo tikiswa ardhi kwa mtikiso, |
5. |
Na milima itapo sagwasagwa, |
6. |
Iwe mavumbi yanayo peperushwa, |
7. |
Na nyinyi mtakuwa namna tatu:- |
8. |
Basi watakuwepo wa kuliani; je, ni wepi wa kuliani? |
9. |
Na wa kushotoni; je, ni wepi wa kushotoni? |
10. |
Na wa mbele watakuwa mbele. |
11. |
Hao ndio watakao karibishwa |
12. |
Katika Bustani zenye neema. |
13. |
Fungu kubwa katika wa mwanzo, |
14. |
Na wachache katika wa mwisho. |
15. |
Watakuwa juu ya viti vya fakhari vilivyo tonewa. |
16. |
Wakiviegemea wakielekeana. |
17. |
Wakitumikiwa na wavulana wa ujana wa milele, |
18. |
Kwa vikombe na mabirika na bilauri za vinywaji kutoka chemchem safi. |
19. |
Hawataumwa kichwa kwa vinywaji hivyo wala hawatoleweshwa. |
20. |
Na matunda wayapendayo, |
21. |
Na nyama za ndege kama wanavyo tamani. |
22. |
Na Mahurulaini, |
23. |
Walio kama mfano wa lulu zilio hifadhiwa. |
24. |
Ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda. |
25. |
Humo hawatasikia porojo wala maneno ya dhambi, |
26. |
Isipo kuwa maneno ya Salama, Salama. |
27. |
Na wale wa mkono wa kulia, ni yepi yatakuwa ya wa kuliani? |
28. |
Katika mikunazi isiyo na miba, |
29. |
Na migomba iliyo pangiliwa, |
30. |
Na kivuli kilicho tanda, |
31. |
Na maji yanayo miminika, |
32. |
Na matunda mengi, |
33. |
Hayatindikii wala hayakatazwi, |
34. |
Na matandiko yaliyo nyanyuliwa. |
35. |
Hakika Sisi tutawaumba (Mahurulaini) upya, |
36. |
Na tutawafanya vijana, |
37. |
Wanapendana na waume zao, hirimu moja. |
38. |
Kwa ajili ya watu wa kuliani. |
39. |
Fungu kubwa katika wa mwanzo, |
40. |
Na fungu kubwa katika wa mwisho. 3 |
41. |
Na watu wa kushotoni; je ni yepi ya wa kushotoni? |
42. |
Katika upepo wa moto, na maji yanayo chemka, |
43. |
Na kivuli cha moshi mweusi, |
44. |
Si cha kuburudisha wala kustarehesha. |
45. |
Hakika hao walikuwa kabla ya haya wakiishi maisha ya anasa. |
46. |
Na walikuwa wakishikilia kufanya madhambi makubwa, |
47. |
Na walikuwa wakisema: Tutakapo kufa na tukawa udongo na mafupa, ati ndio tutafufuliwa? |
48. |
Au baba zetu wa zamani? |
49. |
Sema: Hakika wa zamani na wa mwisho |
50. |
Bila ya shaka watakusanywa kwa wakati wa siku maalumu. |
51. |
Kisha nyinyi, mlio potea, mnao kanusha, |
52. |
Kwa yakini mtakula mti wa Zaqqumu. |
53. |
Na kwa mti huo mtajaza matumbo. |
54. |
Na juu yake mtakunywa maji yanayo chemka. |
55. |
Tena mtakunywa kama wanavyo kunywa ngamia wenye kiu. |
56. |
Hiyo ndiyo karamu yao Siku ya Malipo. |
57. |
Sisi tumekuumbeni; basi hamsadiki? |
58. |
Je! Mnaiona mbegu ya uzazi mnayo idondokeza? |
59. |
Je! Mnaiumba nyinyi, au ni Sisi ndio Waumbaji? |
60. |
Sisi tumekuwekeeni mauti; na wala Sisi hatushindwi |
61. |
Kuwaleta wengine badala yenu na kukuumbeni nyinyi kwa umbo msilo lijua. |
62. |
Na bila ya shaka mlikwisha jua umbo la kwanza, basi kwa nini hamkumbuki? |
63. |
Je! Mnaona makulima mnayo yapanda? |
64. |
Je! Ni nyinyi mnayo yaotesha au ni Sisi ndio wenye kuotesha? |
65. |
Tungeli taka tungeli yafanya yakawa mapepe, mkabaki mnastaajabu, |
66. |
Mkisema: Hakika sisi tumegharimika; |
67. |
Bali sisi tumenyimwa. |
68. |
Je! Mnayaona maji mnayo yanywa? |
69. |
Je! Ni nyinyi mnayo yateremsha kutoka mawinguni au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha? |
70. |
Tungeli penda tungeli yafanya ya chumvi. Basi mbona hamshukuru? |
71. |
Je! Mnauona moto mnao uwasha? |
72. |
Ni nyinyi mlio uumba mti wake au Sisi ndio Waumbaji? |
73. |
Sisi tumeufanya uwe ni ukumbusho na manufaa kwa walioko nyikani. |
74. |
Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkuu. |
75. |
Basi naapa kwa maanguko ya nyota, |
76. |
Na hakika bila ya shaka hichi ni kiapo kikubwa, laiti mngeli jua! |
77. |
Hakika hii bila ya shaka ni Qur’ani Tukufu, |
78. |
Katika Kitabu kilicho hifadhiwa. |
79. |
Hapana akigusaye ila walio takaswa. |
80. |
Ni uteremsho unao toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. |
81. |
Ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayapuuza? |
82. |
Na badala ya kushukuru kwa riziki yenu mnafanya kuwa mnakadhibisha? |
83. |
Yawaje basi itakapo fika roho kwenye koo, |
84. |
Na nyinyi wakati huo mnatazama! |
85. |
Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi. |
86. |
Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka yangu, |
87. |
Kwanini hamuirudishi hiyo roho, ikiwa nyinyi mnasema kweli? |
88. |
Basi akiwa miongoni mwa walio karibishwa, |
89. |
Basi ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema. |
90. |
Na akiwa katika watu wa upande wa kulia, |
91. |
Basi ni Salamu kwako uliye miongoni mwa watu wa upande wa kulia. |
92. |
Na ama akiwa katika walio kadhibisha wapotovu, |
93. |
Basi karamu yake ni maji yanayo chemka, |
94. |
Na kutiwa Motoni. |
95. |
Hakika hii ndiyo haki yenye yakini. |
96. |
Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkubwa. |