1. |
Saa imekaribia, na mwezi umepasuka! |
2. |
Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: Huu uchawi tu unazidi kuendelea. |
3. |
Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao. Na kila jambo ni lenye kuthibiti. |
4. |
Na bila ya shaka zimewajia khabari zenye makaripio. |
5. |
Hikima kaamili; lakini maonyo hayafai kitu! |
6. |
Basi jiepushe nao. Siku atakapo ita mwitaji kuliendea jambo linalo chusha; |
7. |
Macho yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige walio tawanyika, |
8. |
Wanamkimbilia mwitaji, na makafiri wanasema: Hii ni siku ngumu. |
9. |
Kabla yao kaumu ya Nuhu walikanusha; wakamkanusha mja wetu, na wakasema ni mwendawazimu, na akakaripiwa. |
10. |
Basi akamwomba Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru! |
11. |
Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayo miminika. |
12. |
Na tukazipasua ardhi kwa chemchem, yakakutana maji kwa jambo lilio kadiriwa. |
13. |
Na tukamchukua kwenye safina ya mbao na kamba. |
14. |
Ikawa inakwenda kwa nadhari yetu, kuwa ni malipo kwa alivyo kuwa amekanushwa. |
15. |
Na bila ya shaka tuliiacha iwe ni Ishara. Lakini je, yupo anaye kumbuka? |
16. |
Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo yangu. |
17. |
Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur’ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anaye kumbuka? |
18. |
Kina A’di walikanusha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu? |
19. |
Hakika Sisi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku korofi mfululizo, |
20. |
Ukiwang’oa watu kama vigogo vya mitende vilio ng’olewa. |
21. |
Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu? |
22. |
Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur’ani nyepesi kufahamika; lakini yupo anaye kumbuka? |
23. |
Thamudi waliwakanusha Waonyaji. |
24. |
Wakasema: Ati tumfuate binaadamu mmoja katika sisi? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotofu na kichaa! |
25. |
Ni yeye tu aliye teremshiwa huo ukumbusho kati yetu sote? Bali huyu ni mwongo mwenye kiburi! |
26. |
Kesho watajua ni nani huyo mwongo mwenye kiburi. |
27. |
Hakika Sisi tutawapelekea ngamia jike ili kuwajaribu, basi watazame tu na ustahamili. |
28. |
Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu ya maji itahudhuriwa na aliye khusika. |
29. |
Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja. |
30. |
Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu! |
31. |
Hakika Sisi tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama mabuwa ya kujengea uwa. |
32. |
Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur’ani iwe nyepesi kwa kukumbuka, lakini yupo akumbukaye? |
33. |
Kaumu Lut’i nao waliwakadhibisha Waonyaji. |
34. |
Hakika Sisi tukawapelekea kimbunga cha vijiwe, isipo kuwa wafuasi wa Lut’i. Hao tuliwaokoa karibu na alfajiri. |
35. |
Kwa neema inayo toka kwetu. Hivyo ndivyo tumlipavyo anaye shukuru. |
36. |
Na hakika yeye aliwaonya adhabu yetu; lakini wao waliyatilia shaka hayo maonyo. |
37. |
Na walimtaka awape wageni wake. Tukayapofua macho yao, na tukawaambia: Onjeni basi adhabu na maonyo yangu! |
38. |
Na iliwafikia wakati wa asubuhi adhabu yangu ya kuendelea. |
39. |
Basi onjeni adhabu na maonyo yangu! |
40. |
Na hakika tumeisahilisha Qur’ani kuikumbuka. Lakini yupo anaye kumbuka? |
41. |
Na Waonyaji waliwafikia watu wa Firauni. |
42. |
Walizikadhibisha Ishara zetu zote, nasi tukawashika kama anavyo shika Mwenye nguvu Mwenye uweza. |
43. |
Je! Makafiri wenu ni bora kuliko hao, au yameandikwa vitabuni kuwa nyinyi hamtiwi makosani? |
44. |
Au ndio wanasema: Sisi ni wengi tutashinda tu. |
45. |
Wingi wao huu utashindwa, na wao watasukumwa nyuma. |
46. |
Bali Saa ya Kiyama ndio miadi yao, na Saa hiyo ni nzito zaidi na chungu zaidi. |
47. |
Hakika wakosefu wamo katika upotofu na wazimu. |
48. |
Siku watakapo kokotwa Motoni kifudifudi waambiwe: Onjeni mguso wa Jahannamu! |
49. |
Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo. |
50. |
Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho. |
51. |
Na bila ya shaka tumekwisha waangamiza wenzenu. Lakini yupo anaye kumbuka? |
52. |
Na kila jambo walilo lifanya limo vitabuni. |
53. |
Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa. |
54. |
Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na mito. |
55. |
Katika makalio ya haki kwa Mfalme Mwenye uweza. |