1. |
Naapa kwa mlima wa T’ur, |
2. |
Na Kitabu kilicho andikwa |
3. |
Katika ngozi iliyo kunjuliwa, |
4. |
Na kwa Nyumba iliyo jengwa, |
5. |
Na kwa dari iliyo nyanyuliwa, |
6. |
Na kwa bahari iliyo jazwa, |
7. |
Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea. |
8. |
Hapana wa kuizuia. |
9. |
Siku zitakapo tikisika mbingu kwa mtikiso, |
10. |
Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa. |
11. |
Basi ole wao siku hiyo hao wanao kadhibisha, |
12. |
Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi. |
13. |
Siku watapo sukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu, |
14. |
(Waambiwe): Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukanusha! |
15. |
Je! Huu ni uchawi, au hamwoni tu? |
16. |
Uingieni, mkistahamili au msistahamili – ni mamoja kwenu. Hakika mnalipwa kwa mliyo kuwa mkiyatenda. |
17. |
Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na neema, |
18. |
Wakifurahi kwa yale aliyo wapa Mola wao Mlezi. Na Mola wao Mlezi atawalinda na adhabu ya Motoni. |
19. |
Kuleni na kunyweni kwa raha kabisa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyatenda. |
20. |
Watakuwa wameegemea juu ya viti vya enzi vilivyo pangwa kwa safu. Na tutawaoza mahuru-l-aini. |
21. |
Na walio amini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja hata kidogo katika vitendo vyao. Kila mtu lazima atapata alicho kichuma. |
22. |
Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyo penda. |
23. |
Watapeana humo bilauri zisio na vinywaji vya kuleta maneno ya upuuzi wala dhambi. |
24. |
Iwe wanawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu zilizomo katika chaza. |
25. |
Wataelekeana wakiulizana. |
26. |
Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa; |
27. |
Basi Mwenyezi Mungu akatufanyia hisani na akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto. |
28. |
Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye tu. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu. |
29. |
Basi kumbusha! Kwani wewe, kwa neema ya Mola wako Mlezi, si kuhani wala mwendawazimu. |
30. |
Au wanasema: Huyu ni mtunga mashairi, tunamtarajia kupatilizwa na dahari. |
31. |
Sema: Tarajieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika kutarajia. |
32. |
Au hizo akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao basi ni watu majeuri tu? |
33. |
Au ndio wanasema: Ameitunga hii! Bali basi tu hawaamini! |
34. |
Basi nawalete masimulizi kama haya ikiwa wao wanasema kweli. |
35. |
Au wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji? |
36. |
Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana na yakini. |
37. |
Au wanazo khazina za Mola wako Mlezi au wao ndio wenye madaraka? |
38. |
Au wanazo ngazi za kusikilizia? Basi huyo msikilizaji wao na alete hoja ilio wazi! |
39. |
Au Yeye Mwenyezi Mungu ana wasichana, na nyinyi ndio mna wavulana? |
40. |
Au wewe unawaomba ujira, na kwa hivyo ndio wanaelemewa na uzito wa gharama? |
41. |
Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wameandika? |
42. |
Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini hao walio kufuru ndio watakao tegeka. |
43. |
Au wanae mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Subhanallah! Ametaksika Mwenyezi Mungu na hao wanao washirikisha naye. |
44. |
Na hata wange ona pande linatoka mbinguni linaanguka wange sema: Ni mawingu yaliyo bebana. |
45. |
Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakapo hilikishwa. |
46. |
Siku ambayo hila zao hazitawafaa hata kidogo, wala wao hawatanusuriwa. |
47. |
Na hakika walio dhulumu watapata adhabu nyengine isiyo kuwa hii, lakini wengi wao hawajui. |
48. |
Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi unapo simama, |
49. |
Na usiku pia mtakase, na zinapo kuchwa nyota. |