1. |
Naapa kwa pepo zinazo tawanya, |
2. |
Na zinazo beba mizigo, |
3. |
Na zinazo kwenda kwa wepesi. |
4. |
Na zinazo gawanya kwa amri, |
5. |
Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka ni kweli, |
6. |
Na kwa hakika malipo bila ya shaka yatatokea. |
7. |
Naapa kwa mbingu zenye njia, |
8. |
Hakika nyinyi bila ya shaka mmo katika kauli inayo khitalifiana. |
9. |
Anageuzwa kutokana na haki mwenye kugeuzwa. |
10. |
Wazushi wameangamizwa. |
11. |
Ambao wameghafilika katika ujinga. |
12. |
Wanauliza: Ni lini hiyo siku ya malipo? |
13. |
Hiyo ni siku watakayo adhibiwa Motoni. |
14. |
Onjeni adhabu yenu! Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyahimiza. |
15. |
Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem. |
16. |
Wanapokea aliyo wapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema. |
17. |
Walikuwa wakilala kidogo tu usiku. |
18. |
Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira. |
19. |
Na katika mali yao ipo haki ya mwenye kuomba na asiye omba. |
20. |
Na katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini. |
21. |
Na pia katika nafsi zenu – Je! Hamwoni? |
22. |
Na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyo ahidiwa. |
23. |
Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, hakika haya ni kweli kama ilivyo kweli kuwa nyinyi mnasema. |
24. |
Je! Imekufikia hadithi ya wageni wa Ibrahim wanao hishimiwa? |
25. |
Walipo ingia kwake wakasema: Salama! Na yeye akasema: Salama! Nyinyi ni watu nisio kujueni. |
26. |
Akenda kwa ahali yake na akaja na ndama aliye nona. |
27. |
Akawakaribisha, akasema: Mbona hamli? |
28. |
Akahisi kuwaogopa katika nafsi yake. Wakasema: Usiwe na khofu, nao wakambashiria kupata kijana mwenye ilimu. |
29. |
Ndipo mkewe akawaelekea, na huku anasema na akijipiga usoni kwa mastaajabu, na kusema: Mimi ni kikongwe na tasa! |
30. |
Wakasema: Ndivyo vivyo hivyo alivyo sema Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mwenye kujua. |
31. |
AKASEMA: Basi ujumbe wenu ni nini, enyi mlio tumwa? |
32. |
Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wakosefu, |
33. |
Tuwatupie mawe ya udongo, |
34. |
Yaliyo tiwa alama kutoka kwa Mola wako Mlezi kwa ajili ya wanao pindukia mipaka. |
35. |
Kwa hivyo tutawatoa katika hao wale walio amini. |
36. |
Lakini hatukupata humo ila nyumba moja tu yenye Waislamu! |
37. |
Na tukaacha humo Ishara kwa ajili ya wanao iogopa adhabu chungu. |
38. |
Na katika khabari za Musa, tulipo mtuma kwa Firauni na hoja wazi. |
39. |
Lakini alipuuza kwa sababu ya nguvu zake na akasema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu! |
40. |
Basi tukamkamata yeye na majeshi yake na tukawatupa baharini, na yeye ndiye wa kulaumiwa. |
41. |
Na katika khabari za A’di tulipo wapelekea upepo wa kukata uzazi. |
42. |
Haukuacha chochote ulicho kifikia ila ulikifanya kama kilio nyambuka. |
43. |
Na katika khabari za Thamudi walipo ambiwa: Jifurahisheni kwa muda mdogo tu. |
44. |
Wakaasi amri ya Mola wao Mlezi. Basi uliwanyakua moto wa radi nao wanaona. |
45. |
Basi hawakuweza kusimama wala hawakuwa wenye kujitetea. |
46. |
Na kaumu ya Nuhu hapo mbele. Hakika hao walikuwa watu wapotovu. |
47. |
Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi bila ya shaka ndio twenye uwezo wa kuzitanua. |
48. |
Na ardhi tumeitandaza; basi watandazaji wazuri namna gani Sisi! |
49. |
Na katika kila kitu tumeumba kwa jozi ili mzingatie. |
50. |
Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake. |
51. |
Wala msifanye kuwa kuna mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake. |
52. |
Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu. |
53. |
Je! Wameambizana kwa haya? Bali hawa ni watu waasi. |
54. |
Basi waachilie mbali, nawe hulaumiwi. |
55. |
Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini. |
56. |
Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi. |
57. |
Na sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe. |
58. |
Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti. |
59. |
Hakika walio dhulumu wana fungu lao la adhabu kama fungu la wenzao. Basi wasinihimize. |
60. |
Ole wao walio ikanusha siku yao waliyo ahidiwa. |