50. Qaaf

1.

Qaaf. Naapa kwa Qur’ani tukufu!

2.

Bali wanastaajabu kwamba amewafikia mwonyaji kutoka miongoni mwao, na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu!

3.

Ati tukifa na tukawa udongo…? Kurejea huko kuko mbali!

4.

Hakika Sisi tunajua kiasi cha kila kinacho punguzwa na ardhi kutokana nao. Na kwetu kipo Kitabu kinacho hifadhi yote.

5.

Lakini waliikanusha Haki ilipo wajia; kwa hivyo wamo katika mambo ya mkorogo.

6.

Je! Hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyo zijenga, na tukazipamba. Wala hazina nyufa.

7.

Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima, na tukaiotesha mimea mizuri ya kila namna.

8.

Yawe haya ni kifumbua macho na ukumbusho kwa kila mja mwenye kuelekea.

9.

Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyo barikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa.

10.

Na mitende mirefu yenye makole yaliyo zaa kwa wingi,

11.

Ili iwe ni riziki kwa waja wangu. Na tukaifufua kwa maji nchi iliyo kuwa imekufa. Kama hivyo ndivyo utakavyo kuwa ufufuaji.

12.

Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuhu na wakaazi wa Rassi na Thamudi.

13.

Na A’di na Firauni na kaumu ya Lut’i.

14.

Na wakaazi wa Machakani, na watu wa Tubbaa’. Wote hao waliwakanusha Mitume, kwa hivyo onyo likathibitika juu yao.

15.

Kwani tulichoka kwa kuumba mara ya kwanza. Bali wao wamo katika shaka tu juu ya umbo jipya.

16.

Na hakika tumemuumba mtu, nasi tunayajua yanayo mpitikia katika nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake.

17.

Wanapo pokea wapokeaji wawili, wanao kaa kuliani na kushotoni.

18.

Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari.

19.

Na uchungu wa kutoka roho utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyo kuwa ukiyakimbia.

20.

Na litapulizwa baragumu. Hiyo ndiyo Siku ya Miadi.

21.

Na kila nafsi itakuja na pamoja nayo mchungaji na shahidi.

22.

(Aambiwe): Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, na kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali.

23.

Na mwenzake atasema: Huyu niliye naye mimi kesha tayarishwa.

24.

Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inda,

25.

Akatazaye kheri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka,

26.

Aliye weka mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi mtupeni katika adhabu kali.

27.

Mwenzake aseme: Ee Mola wetu Mlezi! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali.

28.

(Mwenyezi Mungu) aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikuleteeni mbele onyo langu.

29.

Mbele yangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja wangu.

30.

Siku tutapo iambia Jahannamu: Je! Umejaa? Nayo itasema: Je! Kuna ziada?

31.

Na Pepo italetwa karibu kwa ajili ya wachamngu, haitakuwa mbali.

32.

Haya ndiyo mnayo ahidiwa kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu na akajilinda.

33.

Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema hali kuwa hamwoni, na akaja kwa moyo ulio elekea-

34.

(Ataambiwa) ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima dawamu.

35.

Humo watapata wakitakacho, na kwetu yako ya ziada.

36.

Na kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao walio kuwa na nguvu zaidi kuliko hawa! Nao walitanga tanga katika nchi nyingi. Je! Walipata pa kukimbilia?

37.

Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia.

38.

Na bila ya shaka Sisi tumeziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao mnamo siku sita; na wala hayakutugusa machofu.

39.

Basi vumilia kwa hayo wasemayo, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.

40.

Na katika usiku pia mtakase, na baada ya kusujudu.

41.

Na sikiliza siku atapo nadi mwenye kunadi kutoka pahala karibu.

42.

Siku watakapo sikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kufufuka.

43.

Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo.

44.

Siku itapo wapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi.

45.

Sisi tunajua kabisa wayasemayo. Wala wewe si mwenye kuwatawalia kwa ujabari. Basi mkumbushe kwa Qur’ani anaye liogopa onyo.