1. |
H’a Mim |
2. |
Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha, |
3. |
Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji. |
4. |
Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima, |
5. |
Jambo litokalo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma. |
6. |
Ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua. |
7. |
Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi mna yakini. |
8. |
Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha- Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa mwanzo. |
9. |
Lakini wao wanacheza katika shaka. |
10. |
Basi ingoje siku ambayo mbingu zitakapo leta moshi ulio dhaahiri, |
11. |
Utakao wafunika watu: Hii ni adhabu chungu! |
12. |
Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini. |
13. |
Nini faida ya kukumbuka kwao? Na alikwisha wafikia Mtume mwenye kubainisha. |
14. |
Na wao wakamgeuzia uso, na wakasema: Huyu amefunzwa, naye ni mwendawazimu. |
15. |
Hakika sisi tutaiondoa adhabu kidogo, lakini nyinyi kwa yakini mtarejea vile vile! |
16. |
Siku tutayo yashambulia mashambulio makubwa, bila ya shaka Sisi ni wenye kutesa. |
17. |
Na hakika kabla ya hawa tuliwafanyia mtihani watu wa Firauni, na aliwafikia Mtume Mtukufu. |
18. |
Akasema: Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni Mtume Muaminifu. |
19. |
Na msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu; hakika mimi nitakuleteeni uthibitisho ulio wazi. |
20. |
Nami najikinga kwa Mola wangu Mlezi na ndiye Mola wenu Mlezi pia, ili msinipige mawe. |
21. |
Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami. |
22. |
Ndipo akamwomba Mola wake Mlezi: Hakika watu hawa ni wakosefu. |
23. |
Mwenyezi Mungu akasema: Basi nenda na waja wangu usiku. Kwa yakini mtafuatwa. |
24. |
Na iache bahari vivyo hivyo imeachana, hakika wao hao ni jeshi litakalo zamishwa. |
25. |
Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha! |
26. |
Na mimea na vyeo vitukufu! |
27. |
Na neema walizo kuwa wakijistareheshea! |
28. |
Ndio hivyo! Na tukawarithisha haya watu wenginewe. |
29. |
La mbingu wala ardhi hazikuwalilia, wala hawakupewa muhula. |
30. |
Na bila ya shaka tuliwaokoa Wana wa Israili katika adhabu ya kuwadhalilisha, |
31. |
Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupindukia mipaka. |
32. |
Na tuliwakhiari kwa ujuzi wetu kuliko walimwengu wenginewe. |
33. |
Na tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi. |
34. |
Hakika hawa wanasema: |
35. |
Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi hatufufuliwi. |
36. |
Basi warudisheni baba zetu, ikiwa nyinyi mnasema kweli. |
37. |
Je! Ni wao bora au watu wa Tubbaa’ na walio kuwa kabla yao? Tuliwaangamiza. Hakika hao walikuwa wakosefu. |
38. |
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa mchezo. |
39. |
Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui. |
40. |
Hakika siku ya Uamuzi ni wakati ulio wekwa kwa wao wote. |
41. |
Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa. |
42. |
Isipo kuwa atakaye mrehemu Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. |
43. |
Hakika Mti wa Zaqqum, |
44. |
Ni chakula cha mwenye dhambi. |
45. |
Kama shaba iliyo yayushwa, hutokota matumboni |
46. |
Kama kutokota kwa maji ya moto. |
47. |
(Itasemwa:) Mkamateni na mtupeni katikati ya Jahannamu! |
48. |
Kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayo chemka. |
49. |
Onja! Ati wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu! |
50. |
Hakika haya ndiyo mliyo kuwa mkiyatilia shaka. |
51. |
Hakika wachamngu watakuwa katika mahali pa amani, |
52. |
Katika mabustani na chemchem, |
53. |
Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana, |
54. |
Hivi ndivyo itakavyo kuwa, na tutawaoza mahurilaini. |
55. |
Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani. |
56. |
Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na (Mwenyezi Mungu) atawalinda na adhabu ya Jahannamu, |
57. |
Kuwa ni fadhila zitokazo kwa Mola wako Mlezi. Huko ndiko kufuzu kukubwa. |
58. |
Basi tumeifanya nyepesi hii Qur’ani kwa ulimi wako, ili wapate kukumbuka. |
59. |
Ngoja tu, na wao wangoje pia. |