1. |
Naapa kwa wanao jipanga kwa safu. |
2. |
Na kwa wenye kukataza mabaya. |
3. |
Na kwa wenye kusoma Ukumbusho. |
4. |
Hakika Mungu wenu bila ya shaka ni Mmoja. |
5. |
Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na yaliyomo kati yao, na ni Mola Mlezi wa mashariki zote. |
6. |
Hakika Sisi tumeipamba mbingu ya karibu kwa pambo la nyota. |
7. |
Na kulinda na kila shet’ani a’si. |
8. |
Wasiweze kuwasikiliza viumbe watukufu. Na wanafukuzwa huko kila upande. |
9. |
Wakifurushwa. Na wanayo adhabu ya kudumu. |
10. |
Isipo kuwa anaye nyakua kitu kidogo, na mara humfwatia kimondo kinacho ng’ara. |
11. |
Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tulio waumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unao nata. |
12. |
Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara. |
13. |
Na wanapo kumbushwa hawakumbuki. |
14. |
Na wanapo ona Ishara, wanafanya maskhara. |
15. |
Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi tu ulio dhaahiri. |
16. |
Ati tukisha kufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa? |
17. |
Hata baba zetu wa zamani? |
18. |
Sema: Naam! Hali nanyi ni madhalili. |
19. |
Huko utapigwa ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona! |
20. |
Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo. |
21. |
Hii ndiyo Siku ya Hukumu mliyo kuwa mkiikadhibisha. |
22. |
Wakusanyeni walio dhulumu, na wake zao, na hao walio kuwa wakiwaabudu – |
23. |
Badala ya Mwenyezi Mungu. Waongozeni njia ya Jahannamu! |
24. |
Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa: |
25. |
Mna nini? Mbona hamsaidiani? |
26. |
Bali hii leo, watasalimu amri. |
27. |
Watakabiliana wao kwa wao kuulizana. |
28. |
Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kulia. |
29. |
Watasema (wakubwa): Bali nyinyi wenyewe hamkuwa Waumini. |
30. |
Sisi hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi wenyewe mlikuwa wapotovu. |
31. |
Basi hukumu ya Mola wetu Mlezi imekwisha tuthibitikia. Hakika bila ya shaka tutaonja tu adhabu. |
32. |
Tulikupotezeni kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu. |
33. |
Basi wao kwa hakika siku hiyo watashirikiana katika adhabu pamoja. |
34. |
Hivyo ndivyo tutakavyo wafanyia wakosefu. |
35. |
Wao walipo kuwa wakiambiwa La ilaha illa ‘Llahu Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu tu, wakijivuna. |
36. |
Na wakisema: Hivyo sisi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mtunga mashairi mwendawazimu? |
37. |
Bali huyu amekuja kwa Haki, na amewasadikisha Mitume. |
38. |
Hakika nyinyi bila ya shaka mtaionja adhabu chungu. |
39. |
Wala hamlipwi ila hayo mliyo kuwa mkiyafanya. |
40. |
Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa. |
41. |
Hao ndio watakao pata riziki maalumu, |
42. |
Matunda, nao watahishimiwa. |
43. |
Katika Bustani za neema. |
44. |
Wako juu ya viti wamekabiliana. |
45. |
Wanazungushiwa kikombe chenye kinywaji cha chemchem |
46. |
Kinywaji cheupe, kitamu kwa wanywao. |
47. |
Hakina madhara, wala hakiwaleweshi. |
48. |
Na watakuwa nao wanawake wenye macho ya staha mazuri. |
49. |
Hao wanawake kama mayai yaliyo hifadhika. |
50. |
Waingie kuulizana wenyewe kwa wenyewe. |
51. |
Aseme msemaji mmoja miongoni mwao: Hakika mimi nalikuwa na rafiki |
52. |
Aliye kuwa akinambia: Hivyo wewe ni katika wanao sadiki |
53. |
Ati tukisha kufa tukawa udongo na mafupa, ndio tutalipwa na kuhisabiwa? |
54. |
Atasema: Je! Nyie mnawaona? |
55. |
Basi atachungulia amwone katikati ya Jahannamu. |
56. |
Atasema: Wallahi! Ulikaribia kunipoteza. |
57. |
Na lau kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi bila ya shaka ningeli kuwa miongoni mwa walio hudhurishwa. |
58. |
Je! Sisi hatutakufa, |
59. |
Isipo kuwa kifo chetu cha kwanza? Wala sisi hatutaadhibiwa. |
60. |
Hakika huku bila ya shaka ndiko kufuzu kukubwa. |
61. |
Kwa mfano wa haya nawatende watendao. |
62. |
Je! Kukaribishwa hivi si ndio bora, au mti wa Zaqqum? |
63. |
Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso kwa walio dhulumu. |
64. |
Hakika huo ni mti unao toka katikati ya Jahannamu. |
65. |
Mashada ya matunda yake kama kwamba vichwa vya mashet’ani. |
66. |
Basi hakika bila ya shaka hao watayala hayo, na wajaze matumbo. |
67. |
Kisha juu yake wanyweshwe mchanganyo wa maji yamoto yaliyo chemka. |
68. |
Kisha hakika marejeo yao bila ya shaka yatakuwa kwenye Jahannamu. |
69. |
Hakika waliwakuta baba zao wamepotea. |
70. |
Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao. |
71. |
Na bila ya shaka walikwisha potea kabla yao wengi wa watu wa zamani. |
72. |
Na Sisi hakika tuliwapelekea waonyaji. |
73. |
Basi hebu angalia ulikuwaje mwisho wa walio onywa. |
74. |
Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa. |
75. |
Na hakika Nuhu alitwita, na Sisi ni bora wa waitikiaji. |
76. |
Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa. |
77. |
Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia. |
78. |
Na tukamwachia (sifa njema) kwa walio kuja baadaye. |
79. |
Iwe salama kwa Nuhu ulimwenguni kote! |
80. |
Kwa hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema. |
81. |
Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. |
82. |
Kisha tukawazamisha wale wengine. |
83. |
Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake, |
84. |
Alipo mjia Mola wake Mlezi kwa moyo mzima. |
85. |
Alimwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini? |
86. |
Kwa kuzua tu mnataka miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu? |
87. |
Mnamdhania nini Mola Mlezi wa walimwengu wote? |
88. |
Kisha akapiga jicho kutazama nyota. |
89. |
Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa! |
90. |
Nao wakamwacha, wakampa kisogo. |
91. |
Basi akaiendea miungu yao kwa siri, akaiambia: Mbona hamli? |
92. |
Mna nini hata hamsemi? |
93. |
Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kulia. |
94. |
Basi wakamjia upesi upesi. |
95. |
Akasema: Hivyo mnaviabudu vitu mnavyo vichonga wenyewe? |
96. |
Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni nyinyi na hivyo mnavyo vifanya! |
97. |
Wakasema: Mjengeeni jengo, na kisha mtupeni motoni humo! |
98. |
Basi walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndio wa chini. |
99. |
Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu Mlezi; Yeye ataniongoa. |
100. |
Ewe Mola wangu Mlezi! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema. |
101. |
Basi tukambashiria mwana aliye mpole. |
102. |
Basi alipo fika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyo amrishwa, utanikuta mimi, Inshallah, katika wanao subiri. |
103. |
Basi wote wawili walipo jisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji. |
104. |
Tulimwita: Ewe Ibrahim! |
105. |
Umekwisha itimiliza ndoto. Hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao tenda mema. |
106. |
Hakika haya ni majaribio yaliyo dhaahiri. |
107. |
Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu. |
108. |
Na tukamwachia (sifa njema) kwa watu walio kuja baadaye. |
109. |
Iwe salama kwa Ibrahim! |
110. |
Hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema. |
111. |
Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. |
112. |
Na tukambashiria kuzaliwa Is-haqa, naye ni Nabii miongoni mwa watu wema. |
113. |
Na tukambarikia yeye na Is-haqa. Na miongoni mwa dhuriya zao walitokea wema na wenye kudhulumu nafsi zao waziwazi. |
114. |
Na kwa hakika tuliwafanyia hisani Musa na Haruni. |
115. |
Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na dhiki kubwa. |
116. |
Na tukawanusuru; na wakawa wao ndio wenye kushinda. |
117. |
Na tukawapa wawili hao Kitabu kinacho bainisha. |
118. |
Na tukawaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka. |
119. |
Na tukawaachia (sifa njema) katika watu walio kuja baadaye. |
120. |
Iwe salama kwa Musa na Haruni! |
121. |
Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema. |
122. |
Hakika wawili hao ni katika waja wetu walio amini. |
123. |
Na hakika Ilyas bila ya shaka alikuwa miongoni mwa Mitume. |
124. |
Alipo waambia watu wake: Hamwogopi? |
125. |
Mnamwomba Baa’li na mnamwacha Mbora wa waumbaji, |
126. |
Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa zamani? |
127. |
Wakamkadhibisha. Basi kwa hakika watahudhurishwa; |
128. |
Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa. |
129. |
Na tumemwachia (sifa nzuri) kwa walio kuja baadaye. |
130. |
Iwe salama kwa Ilyas. |
131. |
Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema. |
132. |
Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. |
133. |
Na hakika Lut’i bila ya shaka ni miongoni mwa Mitume. |
134. |
Tulipo mwokoa yeye na ahali zake wote, |
135. |
Isipo kuwa mwanamke mkongwe katika wale walio bakia nyuma. |
136. |
Kisha tukawaangamiza wale wengineo. |
137. |
Na hakika nyinyi mnawapitia wakati wa asubuhi, |
138. |
Na usiku. Basi je! Hamyatii akilini? |
139. |
Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa Mitume. |
140. |
Alipo kimbia katika jahazi lilio sheheni. |
141. |
Akaingia katika kupigiwa kura, na akawa katika walio shindwa. |
142. |
Samaki akammeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa. |
143. |
Na ingeli kuwa hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu, |
144. |
Bila ya shaka angeli kaa ndani yake mpaka siku ya kufufuliwa. |
145. |
Lakini tulimtupa ufukweni patupu, hali yu mgonjwa. |
146. |
Na tukauotesha juu yake mmea wa kabila ya mung’unye. |
147. |
Na tulimtuma kwa watu laki moja au zaidi. |
148. |
Basi wakaamini, na tukawastarehesha kwa muda. |
149. |
Basi waulize: Ati Mola wako Mlezi ndiye mwenye watoto wa kike, na wao wanao watoto wa kiume? |
150. |
Au tumewaumba Malaika kuwa ni wanawake, na wao wakashuhudia? |
151. |
Ati ni kwa uzushi wao ndio wanasema: |
152. |
Mwenyezi Mungu amezaa! Ama hakika bila ya shaka hao ni waongo! |
153. |
Ati amekhiari watoto wa kike kuliko wanaume? |
154. |
Mna nini? Mnahukumu vipi nyinyi? |
155. |
Hamkumbuki? |
156. |
Au mnayo hoja iliyo wazi? |
157. |
Basi leteni Kitabu chenu kama mnasema kweli. |
158. |
Na wameweka makhusiano ya nasaba baina yake na majini; na majini wamekwisha jua bila ya shaka kuwa wao watahudhurishwa. |
159. |
Subhana ‘Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo msingizia. |
160. |
Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa. |
161. |
Basi hakika nyinyi na mnao waabudu |
162. |
Hamwezi kuwapoteza |
163. |
Isipo kuwa yule atakaye ingia Motoni. |
164. |
Na hapana katika sisi ila anapo mahali pake maalumu. |
165. |
Na hakika bila ya shaka sisi ndio wajipangao safu. |
166. |
Na hakika sisi ndio wenye kusabihi kutakasa. |
167. |
Na walikuwapo walio kuwa wakisema: |
168. |
Tungeli kuwa na Ukumbusho kama wa watu wa zamani, |
169. |
Bila ya shaka tungeli kuwa ni waja wa Mwenyezi Mungu wenye ikhlasi. |
170. |
Lakini waliukataa. Basi watakuja jua. |
171. |
Na bila ya shaka neno letu lilikwisha tangulia kwa waja wetu walio tumwa. |
172. |
Ya kuwa wao bila ya shaka ndio watakao nusuriwa. |
173. |
Na kwamba jeshi letu ndilo litakalo shinda. |
174. |
Basi waachilie mbali kwa muda. |
175. |
Na watazame, nao wataona. |
176. |
Je! Wanaihimiza adhabu yetu? |
177. |
Basi itakapo shuka uwanjani kwao, itakuwa asubuhi mbaya kwa walio onywa. |
178. |
Na waache kwa muda. |
179. |
Na tazama, na wao wataona. |
180. |
Subhana Rabbi’l’Izzat Ametakasika Mola Mlezi Mwenye enzi na yale wanayo mzulia. |
181. |
Na Salamu juu ya Mitume. |
182. |
Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote. |