1. |
Ewe Nabii! Mche Mwenyezi Mungu wala usiwat’ii makafiri na wanaafiki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima. |
2. |
Na fuata uliyo funuliwa kwa wahyi kutokana na Mola wako Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari ya mnayo yatenda. |
3. |
Na mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutegemewa. |
4. |
Mwenyezi Mungu hakumwekea mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake. Wala hakuwafanya wake zenu – ambao mnawalinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu – kuwa ni mama zenu. Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu khasa. Hayo ni maneno ya vinywa vyenu tu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye sema kweli, naye ndiye anaye ongoa Njia. |
5. |
Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa hamwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki zenu. Wala si lawama juu yenu kwa mlivyo kosea. Lakini ipo lawama katika yale ziliyo fanya nyoyo zenu kwa makusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. |
6. |
Nabii ni bora zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Na wake zake ni mama zao. Na jamaa ni karibu wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu kuliko Waumini wengine na Wahamiaji. Ila muwe mnawafanyia wema marafiki zenu. Haya yamekwisha andikwa Kitabuni. |
7. |
Na tulipo chukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe, na Nuhu na Ibrahim na Isa mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu, |
8. |
Ili (Mwenyezi Mungu) awaulize wakweli juu ya ukweli wao. Na amewaandalia makafiri adhabu chungu. |
9. |
Enyi mlio amini! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yenu. Pale yalipo kufikilieni majeshi, nasi tukayapelekea upepo, na majeshi msiyo yaona. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda. |
10. |
Walipo kujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu; na macho yalipo kodoka, na nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbali mbali. |
11. |
Hapo ndipo Waumini walipo jaribiwa, na wakatikiswa mtikiso mkali. |
12. |
Na walipo sema wanaafiki na wale wenye maradhi katika nyoyo zao: Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawakutuahidi ila udanganyifu tu. |
13. |
Na kundi moja katika miongoni mwao lilipo sema: Enyi watu wa Yathrib! Hapana kukaa nyinyi! Rudini. Na kundi jingine miongoni mwao likaomba ruhusa kwa Mtume kwa kusema: Hakika nyumba zetu ni tupu. Wala hazikuwa tupu; hawakutaka ila kukimbia tu. |
14. |
Na lau kuwa wangeli ingiliwa kwa pande zote, kisha wakatakiwa kufanya khiana, wangeli fanya, na wasingeli sita ila kidogo tu. |
15. |
Na hakika walikwisha muahidi Mwenyezi Mungu kabla yake kwamba hawatageuza migongo yao. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa. |
16. |
Sema: Kukimbia hakukufaeni kitu ikiwa mnakimbia mauti au kuuwawa, na hata hivyo hamtastareheshwa ila kidogo tu. |
17. |
Sema: Ni nani wa kukulindeni na Mwenyezi Mungu pindi akikutakieni uovu, au akikutakieni rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu. |
18. |
Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawajua hao wanao zuilia, na wanao waambia ndugu zao: Njooni kwetu! Wala hawaingii vitani ila kidogo tu. |
19. |
Wana choyo juu yenu. Ikifika khofu utawaona wanakutazama na macho yao yanazunguka, kama yule ambaye aliye zimia kwa kukaribia mauti. Na khofu ikiondoka wanakuudhini kwa ndimi kali, nao ni mabakhili kwa kila la kheri. Hao hawakuamini, basi Mwenyezi Mungu amevibat’ilisha vitendo vyao. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. |
20. |
Wanafikiri yale makundi ya maadui hayajaondoka. Na yakija hayo makundi watatamani laiti wao wako majangwani pamoja na mabedui, wakiuliza khabari zenu. Na lau wakiwa pamoja nanyi hawapigani ila kidogo tu. |
21. |
Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana. |
22. |
Na Waumini walipo yaona makundi, walisema: Haya ndiyo aliyo tuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli. Na hayo hayakuwazidisha ila Imani na ut’iifu. |
23. |
Miongoni mwa Waumini wapo watu walio timiza waliyo ahidiana na Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo. |
24. |
Ili Mwenyezi Mungu awalipe wakweli kwa sababu ya ukweli wao, na awaadhibu wanaafiki pindi akitaka, au apokee toba yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. |
25. |
Na Mwenyezi Mungu aliwarudisha nyuma makafiri juu ya ghadhabu yao; hawakupata kheri yoyote. Na Mwenyezi Mungu amewatosheleza Waumini katika vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na uweza. |
26. |
Na akawateremsha wale walio wasaidia (maadui) katika Watu wa Kitabu kutoka katika ngome zao; na akatia khofu katika nyoyo zao. Baadhi yao mkawa mnawauwa, na wengine mnawateka. |
27. |
Na akakurithisheni ardhi zao na nyumba zao na mali zao, na ardhi msiyo pata kuikanyaga. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. |
28. |
Ewe Nabii! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka maisha ya dunia na pambo lake, basi njooni, nitakupeni kitoka nyumba, na kukuacheni mwachano mzuri. |
29. |
Na ikiwa mnamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya Akhera, basi Mwenyezi Mungu amewaandalia wafanyao mema, miongoni mwenu, malipo makubwa. |
30. |
Enyi wake wa Nabii! Atakaye fanya uchafu dhaahiri miongoni mwenu, atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. |
31. |
NA MIONGONI mwenu atakeye mt’ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akatenda mema, tutampa malipo yake mara mbili, na tutamwandalia riziki ya ukarimu. |
32. |
Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha Mungu basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema. |
33. |
Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijahilia ya kizamani. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt’iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukusafisheni baarabara. |
34. |
Na kumbukeni yasomwayo majumbani mwenu katika Aya za Mwenyezi Mungu na hikima. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo ya siri, na Mwenye khabari. |
35. |
Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na wat’iifu wanaume na wat’iifu wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanao subiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na wanao funga wanaume na wanawake, na wanao jihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanao mdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa. |
36. |
Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapo kata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi. |
37. |
Na ulipo mwambia yule Mwenyezi Mungu aliye mneemesha, nawe ukamneemesha: Shikamana na mkeo, na mche Mwenyezi Mungu. Na ukaficha nafsini mwako aliyo taka Mwenyezi Mungu kuyafichua, nawe ukawachelea watu, hali Mwenyezi Mungu ndiye mwenye haki zaidi kumchelea. Basi Zaid alipo kwisha haja naye tulikuoza wewe, ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kupanga watapo kuwa wamekwisha timiza nao shuruti za t’alaka. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kutekelezwa. |
38. |
Hapana ubaya kwa Nabii kufanya aliyo mhalalishia Mwenyezi Mungu. Huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa walio pita zamani. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni kudura iliyo kwisha kadiriwa. |
39. |
(Hao wa zamani) walio kuwa wakifikisha risala za Mwenyezi Mungu na wanamwogopa Yeye, na wala hawamwogopi yeyote isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ndiye atoshaye kuhisabu. |
40. |
Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. |
41. |
Enyi mlio amini! Mdhukuruni Mwenyezi Mungu kwa wingi wa kumdhukuru. . |
42. |
Na mtakaseni asubuhi na jioni. |
43. |
Yeye na Malaika wake ndio wanakurehemuni ili kukutoeni gizani mwende kwenye nuru. Naye ni Mwenye kuwarehemu Waumini. |
44. |
Maamkiano yao siku ya kukutana naye yatakuwa: Salama! Na amewaandalia malipo ya ukarimu. |
45. |
Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na mwonyaji, |
46. |
Na mwitaji kumwendea Mwenyezi Mungu kwa idhini yake, na taa yenye kutoa nuru. |
47. |
Na wabashirie Waumini ya kwamba wana fadhila kubwa inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. |
48. |
Wala usiwat’ii makafiri na wanaafiki, na usijali udhia wao. Nawe mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa. |
49. |
Enyi mlio amini! Mkiwaoa wanawake, Waumini, kisha mkawapa t’alaka kabla ya kuwagusa, basi hamna eda juu yao mtakayo ihisabu. Basi wapeni cha kuwaliwaza, na muwawache kwa kuwachana kwa wema. |
50. |
Ewe Nabii! Tumekuhalalishia wake zako ulio wapa mahari yao, na ulio wamiliki kwa mkono wako wa kulia katika alio kupa Mwenyezi Mungu, na mabinti ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa dada za mama yako walio hama pamoja nawe; na mwanamke Muumini akijitoa mwenyewe kwa Nabii, kama mwenyewe Nabii akitaka kumwoa. Ni halali kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine. Sisi tunajua tuliyo wafaridhia wao katika wake zao na wanawake ilio wamiliki mikono yao ya kulia. Ili isiwe dhiki kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. |
51. |
Unaweza kuakhirisha zamu kwa umtakaye katika wao, na umsogeze umtakaye. Na kama ukimtaka yule uliye mtenga, basi si vibaya kwako. Kufanya hivi kutapelekea yaburudike macho yao, wala wasihuzunike, na wawe radhi juu ya kile unacho wapa wao wote. Na Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo nyoyoni mwenu, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima. |
52. |
Baada ya hawa hawakuhalalikii wewe wanawake wengine, wala kuwabadilisha kwa wake wengine ingawa uzuri wao ukikupendeza; isipo kuwa yule uliye mmiliki kwa mkono wako wa kulia. Na Mwenyezi Mungu anachungua kila kitu. |
53. |
Enyi mlio amini! Msiingie nyumba za Nabii ila mpewe ruhusa kwenda kula, sio kungojea kiwive. Lakini mtakapo itwa basi ingieni, na mkisha kula tawanyikeni, wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii naye anakustahini, lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa jambo la haki. Na mnapo wauliza wakeze haja waulizeni nyuma ya mapazia. Hivyo ndio usafi zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao. Wala haikufalieni kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa wake zake baada yake kabisa. Hakika jambo hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. |
54. |
Mkidhihirisha chochote kile, au mkikificha, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu. |
55. |
Hapana ubaya kwao (wake za Mtume) kuonana na baba zao, wala watoto wao, wala ndugu zao, wala watoto wa ndugu zao wanaume, wala watoto wa ndugu zao wanawake, wala wanawake wenzao, wala wale iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Na enyi wanawake, mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushuhudia kila kitu. |
56. |
Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Nabii. Enyi mlio amini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu. |
57. |
Hakika wanao muudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu amewalaani duniani na Akhera, na amewaandalia adhabu ya kufedhehi. |
58. |
Na wale wanao waudhi Waumini wanaume na wanawake pasina wao kufanya kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilio dhaahiri. |
59. |
Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. |
60. |
Kama wanaafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na waenezao fitna katika Madina hawatoacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda mchache tu. |
61. |
Wamelaanika! Popote watakapo onekana watakamatwa na watauliwa kabisa. |
62. |
Hii ni ada ya Mwenyezi Mungu iliyo kuwa kwa wale walio pita zamani. Wala hutapata mabadiliko katika ada ya Mwenyezi Mungu. |
63. |
Watu wanakuuliza khabari ya Saa (ya Kiyama). Sema: Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu. Na nini kitakujuvya? Pengine hiyo Saa iko karibu. |
64. |
Hakika Mwenyezi Mungu amewalaani makafiri na amewaandalia Moto unao waka kwa nguvu. |
65. |
Watadumu humo milele. Hawampati mlinzi wala wa kuwanusuru. |
66. |
Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema: Laiti tungeli mt’ii Mwenyezi Mungu, na tungeli mt’ii Mtume! |
67. |
Na watasema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tuliwat’ii bwana zetu na wakubwa wetu; nao ndio walio tupoteza njia. |
68. |
Mola wetu Mlezi! Wape wao adhabu mara mbili, na uwalaani laana kubwa. |
69. |
Enyi mlio amini! Msiwe kama wale walio mtaabisha Musa, lakini Mwenyezi Mungu akamtakasa na waliyo yasema, naye alikuwa mwenye hishima mbele ya Mwenyezi Mungu. |
70. |
Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni maneno ya sawasawa. |
71. |
Apate kukutengenezeeni vitendo vyenu na akusameheni madhambi yenu. Na anaye mt’ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, bila ya shaka amefanikiwa mafanikio makubwa. |
72. |
Kwa hakika Sisi tulikadimisha amana kwa mbingu na ardhi na milima; na vyote hivyo vikakataa kuichukua na vikaogopa. Lakini mwanaadamu akaichukua. Hakika yeye amekuwa dhaalimu mjinga. |
73. |
Kwa hivyo Mwenyezi Mungu anawaadhibu wanaafiki wanaume, na wanaafiki wanawake, na washirikina wanaume, na washirikina wanawake; na anawapokelea toba Waumini wanaume, na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. |