26. Ash-Shua’raa

1.

T’aa Siin Miim. (T’.S.M.)

2.

Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.

3.

Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini.

4.

Tunge penda tungeli wateremshia kutoka mbinguni Ishara zikanyenyekea shingo zao.

5.

Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman ila wao hujitenga nao.

6.

Kwa yakini wamekanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia khabari za yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha.

7.

Je! Hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri?

8.

Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

9.

Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

10.

Na Mola wako Mlezi, alipo mwita Musa, akamwambia: Fika kwa watu madhaalimu,

11.

Watu wa Firauni. Hawaogopi?

12.

Akasema: Hakika mimi nachelea wasinikanushe.

13.

Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun.

14.

Na wao wana kisasi juu yangu, kwa hivyo naogopa wasije kuniuwa.

15.

Akasema: Siyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza.

16.

Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

17.

Waachilie Wana wa Israili wende nasi.

18.

(Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi?

19.

Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani?

20.

(Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa miongoni mwa wale walio potea.

21.

Basi nikakukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu Mlezi akanitunukia hukumu, na akanijaalia niwe miongoni mwa Mitume.

22.

Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili?

23.

Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote?

24.

Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini.

25.

(Firauni) akawaambia walio mzunguka: Hamsikilizi?

26.

(Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza.

27.

(Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliye tumwa kwenu ni mwendawazimu.

28.

(Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini.

29.

(Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani.

30.

Akasema: Je! Ijapo kuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi?

31.

Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli.

32.

Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri.

33.

Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao.