1. |
Ametukuka aliye teremsha Furqani kwa mja wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote. |
2. |
Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na mwana, wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa kipimo. |
3. |
Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali hiyo inaumbwa, haijimilikii nafsi zao madhara wala manufaa, wala haimiliki mauti, wala uhai, wala kufufuka. |
4. |
Na wamesema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uzushi alio uzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine! Hakika hawa wamekuja na dhulma na uwongo. |
5. |
Na wakasema: Hivi ni visa vya watu wa kale alivyo viandikisha, anavyo somewa asubuhi na jioni. |
6. |
Sema: Ameyateremsha haya ajuaye siri za katika mbingu na ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. |
7. |
Na wakasema: Ana nini Mtume huyu? Anakula chakula, na anatembea masokoni! Mbona hakuteremshiwa Malaika akawa mwonyaji pamoja naye? |
8. |
Au akaangushiwa khazina juu yake, au akawa na bustani ale katika hiyo? Wakasema madhaalimu: Nyinyi hamumfuati ila mtu aliye rogwa. |
9. |
Tazama jinsi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea, wala hawataiweza Njia. |
10. |
Ametukuka ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko hayo, nayo ni mabustani yapitayo mito kati yao, na atakujaalia majumba ya fakhari. |
11. |
Bali wanaikanusha Saa (ya Kiyama). Na Sisi tumemuandalia Moto mkali kabisa huyo mwenye kuikanusha Saa.. |
12. |
Ule Moto ukiwaona tangu mahali mbali wao watasikia hasira yake na mngurumo wake. |
13. |
Na watakapo tupwa humo mahali dhiki, hali wamefungwa, wataomba wafe. |
14. |
Msiombe kufa mara moja tu, bali mfe mara nyingi! |
15. |
Sema: Je! Haya ni bora au Pepo ya milele, ambayo wameahidiwa wachamngu, iwe kwao malipo na marejeo? |
16. |
Watayapata humo wayatakayo daima dawamu. Hii ni ahadi juu ya Mola wako Mlezi, inayo ombwa. |
17. |
Na siku atakapo wakusanya wao na hao wanao waabudu, na akasema: Je! Ni nyinyi mlio wapoteza waja wangu hawa, au wao wenyewe walipotea njia? |
18. |
Watasema: Subhanak, Umetakasika na upungufu! Haikutupasia sisi kuchukulia walinzi badala yako, lakini Wewe uliwastarehesha wao na baba zao hata wakasahau kukumbuka, na wakawa watu walio angamia. |
19. |
Basi walikukanusheni kwa mliyo yasema. Kwa hivyo hamwezi kujiondolea wala kujisaidia. Na atakaye dhulumu miongoni mwenu tutamwonjesha adhabu kubwa. |
20. |
Na hatukuwatuma kabla yako Mitume wowote ila kwa hakika na yakini walikuwa wakila chakula, na wakenda masokoni. Na tumewajaalia baadhi yenu wawe ni majaribio kwa wengine; je! Mtasubiri? Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuona. |
21. |
NA WALISEMA wale wasio taraji kukutana nasi: Mbona sisi hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu Mlezi? Kwa yakini hawa wamejiona bora nafsi zao, na wamepanda kichwa vikubwa mno! |
22. |
Siku watakayo waona Malaika haitakuwa furaha siku hiyo kwa wakosefu. Na watasema: Mungu apishe mbali! |
23. |
Na tutayaendea yale waliyo yatenda katika vitendo vyao, tuvifanye kama mavumbi yaliyo tawanyika. |
24. |
Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makaazi bora na mahali penye starehe nzuri. |
25. |
Na siku zitapo funguka mbingu kwa mawingu, na wateremshwe Malaika kwa wingi, |
26. |
Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Arrahman, Mwingi wa Rehema, na itakuwa siku ngumu kwa makafiri. |
27. |
Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema: Laiti ningeli shika njia pamoja na Mtume! |
28. |
Ee Ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki! |
29. |
Amenipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwisha nijia, na kweli Shet’ani ni khaini kwa mwanaadamu. |
30. |
Na Mtume alikuwa akisema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur’ani ni kihame. |
31. |
Na vivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu, na Mola wako Mlezi anatosha kuwa Mwenye kuongoa na Mwenye kunusuru. |
32. |
Na wakasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur’ani kwa jumla moja? Hayo ni hivyo ili tuuthibitishe moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu. |
33. |
Wala hawatakuletea mfano wowote, ila na Sisi tutakuletea (jawabu) kwa haki, na tafsiri iliyo bora. |
34. |
Wale ambao watakao kusanywa na kubururwa kifudifudi mpaka kwenye Jahannamu, hao watakuwa na mahali pabaya, ndio wenye kuipotea sana njia. |
35. |
Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa waziri. |
36. |
Tukawaambia: Nendeni kwa watu walio kanusha Ishara zetu. Basi tukawateketeza kabisa. |
37. |
Na watu wa Nuhu, walipo wakanusha Mitume, tuliwazamisha, na tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia wenye kudhulumu adhabu chungu. |
38. |
Na tuliwaangamiza kina A’di na Thamudi na watu wa Rass na vizazi vingi vilivyo kuwa kati yao. |
39. |
Na wote tuliwapigia mifano, na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa. |
40. |
Na kwa yakini wao wanafika kwenye nchi ilio teremshiwa mvua mbaya. Basi, je, hawakuwa wakiiona? Bali walikuwa hawataraji kufufuliwa. |
41. |
Na wanapo kuona hawakuchukulii ila ni mzaha tu, na (wanasema): Ati ndiye huyu Mwenyezi Mungu aliye mtuma kuwa Mtume? |
42. |
Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza tuiache miungu yetu, ingeli kuwa hatukushikamana nayo kwa kuvumilia. Bado watakuja jua, watakapo iona adhabu, ni nani aliye potea njia. |
43. |
Je! Umemwona aliye yafanya matamanio yake kuwa ndio mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake? |
44. |
Au wewe unadhani kwamba wengi wao wanasikia au wanaelewa? Hao hawakuwa ila ni kama nyama hoa tu, bali wao wamepotea zaidi njia. |
45. |
Je! Huoni jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza kivuli. Na angeli taka angeli kifanya kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa ni kiongozi wake. |
46. |
Kisha tunakivutia kwetu kidogo kidogo. |
47. |
Naye ndiye aliye kufanyieni usiku kuwa ni vazi, na usingizi kuwa mapumziko, na akakufanyieni mchana ni kufufuka. |
48. |
Naye ndiye anaye zituma pepo kuwa bishara njema kabla ya rehema yake, na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi. |
49. |
Ili kwa hayo tuihuishe nchi iliyo kufa, na tuwanyweshe wanyama na watu wengi tulio waumba. |
50. |
Na kwa yakini tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka. Lakini watu wengi wanakataa ila kukufuru. |
51. |
Na tungeli taka tungeli peleka katika kila mji Mwonyaji. |
52. |
Basi usiwat’ii makafiri. Na pambana nao kwayo kwa Jihadi kubwa. |
53. |
Naye ndiye aliye zipeleka bahari mbili, hii tamu mno, na hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho. |
54. |
Naye ndiye aliye muumba mwanaadamu kutokana na maji, akamjaalia kuwa na nasaba na ushemeji. Na Mola wako Mlezi ni Muweza. |
55. |
Na wanayaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yasiyo wafaa wala yasiyo wadhuru. Na kafiri daima ni msaidizi wa kumpinga Mola wake Mlezi. |
56. |
Nasi hatukukutuma ila kuwa ni Mbashiri na Mwonyaji. |
57. |
Sema: Sikukuombeni ujira juu yake; ila atakaye na ashike njia iendayo kwa Mola wake Mlezi. |
58. |
Na mtegemee Aliye Hai, ambaye hafi. Na umtukuze kwa sifa zake. Na yatosha kwake kuwa yeye ni Mwenye khabari za dhambi za waja wake. |
59. |
Ambaye ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo ndani yake kwa siku sita. Kisha akatawala juu ya A’rshi, Arrahman, Mwingi wa Rehema! Uliza khabari zake kwa wamjuaye. |
60. |
Na wanapo ambiwa: Msujudieni Arrahman! Wao husema: Ni nani Arrahman? Je! Tumsujudie unaye tuamrisha wewe tu? Na huwazidishia chuki. |
61. |
Ametukuka aliye zijaalia nyota mbinguni, na akajaalia humo taa na mwezi unao ng’ara. |
62. |
Naye ndiye aliye fanya usiku na mchana kufuatana kwa nafuu ya anaye taka kukumbuka, au anaye taka kushukuru. |
63. |
Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanao tembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama! |
64. |
Na wale wanao kesha kwa ajili ya Mola wao Mlezi kwa kusujudu na kusimama. |
65. |
Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu ya Jahannamu. Hakika adhabu yake ikimpata mtu haimwachi. |
66. |
Hakika hiyo ni kituo na makao mabaya. |
67. |
Na wale ambao wanapo tumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo. |
68. |
Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki, wala hawazini – na atakaye fanya hayo atapata madhara, |
69. |
Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa kufedheheka. |
70. |
Isipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. |
71. |
Na aliye tubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Mwenyezi Mungu. |
72. |
Na wale ambao hawatoi ushahidi wa uwongo, na pindi wapitapo penye upuuzi, hupita kwa hishima yao. |
73. |
Na wale ambao wanapo kumbushwa Ishara za Mola wao Mlezi hawajifanyi viziwi nazo, na vipofu. |
74. |
Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu. |
75. |
Hao ndio watakao lipwa makao ya juu kwa kuwa walisubiri, na watakuta humo maamkio na salamu. |
76. |
Wadumu humo – kituo na makao mazuri kabisa. |
77. |
Sema: Mola wangu Mlezi asinge kujalini lau kuwa si kuomba kwenu. Lakini nyinyi mmemkadhibisha. Basi adhabu lazima iwe. |