1. |
Alif Lam Ra. (A.L.R). Hizi ni Aya za Kitabu na Qur’ani inayo bainisha. |
2. |
HUENDA ikawa walio kufuru wakatamani wange kuwa Waislamu. |
3. |
Waache wale, na wastarehe, na iwazuge tamaa. Watakuja jua. |
4. |
Na hatukuuangamiza mji wowote ule ila ulikuwa na muda wake maalumu. |
5. |
Hawawezi watu wowote kuitangulia ajali yao, wala kuchelewa. |
6. |
Na walisema: Ewe uliyeteremshiwa Ukumbusho! Hakika wewe ni mwendawazimu. |
7. |
Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli? |
8. |
Sisi hatuwateremshi Malaika ila kwa sababu ya haki, na hapo hawatapewa muhula. |
9. |
Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda. |
10. |
Na hakika tulikwisha watumia Mitume mataifa ya mwanzo. |
11. |
Na hakuwafikia Mtume ila walimkejeli. |
12. |
Na kama hivi ndivyo tunavyo ingiza katika nyoyo za wakosefu. |
13. |
Hawayaamini haya, na hali ya kuwa umekwisha wapitia mfano wa watu wa kale. |
14. |
Na lau tungeli wafungulia mlango wa mbingu, wakawa wanapanda, |
15. |
Basi wangeli sema: Macho yetu yamelevywa, bali sisi wenyewe tumerogwa. |
16. |
Na hakika tumeweka katika mbingu vituo vya sayari, na tumezipamba kwa wenye kuangalia. |
17. |
Na tumezilinda na kila shetani afukuzwaye. |
18. |
Isipo kuwa mwenye kusikiliza kwa kuibia, naye hufuatwa na kijinga cha moto kinacho onekana. |
19. |
Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake. |
20. |
Na tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku. |
21. |
Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu. |
22. |
Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na tunateremsha kutoka mbinguni maji, kisha tukakunywesheni maji hayo. Wala si nyinyi mnayo yaweka. |
23. |
Na Sisi ndio tunao huisha na tunao fisha. Na Sisi ndio Warithi. |
24. |
Na tunawajua walio tangulia katika nyinyi, na tunawajua walio taakhari. |
25. |
Na hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye wakusanya. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mjuzi. |
26. |
Na tulimuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura. |
27. |
Na majini tuliwaumba kabla kwa moto wa upepo umoto. |
28. |
Na Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura. |
29. |
Basi nitakapo mkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi mumwangukie kumsujudia. |
30. |
Basi Malaika wote pamoja walimsujudia, |
31. |
Isipo kuwa Iblisi. Yeye alikataa kuwa pamoja na walio sujudu. |
32. |
(Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na walio sujudu? |
33. |
Akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu uliye muumba kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yenye sura. |
34. |
(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni maluuni! |
35. |
Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo. |
36. |
Akasema (Iblisi): Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watapo fufuliwa. |
37. |
(Mwenyezi Mungu) akasema: Hakika wewe ni katika walio pewa muhula |
38. |
Mpaka siku ya wakati maalumu. |
39. |
Akasema: Mola wangu Mlezi! Ilivyo kuwa umenitia makosani, basi nahakikisha nitawazaini hapa duniani na nitawapoteza wote, |
40. |
Ila waja wako walio safika. |
41. |
Akasema: Hii Njia ya kujia kwangu Iliyo Nyooka. |
42. |
Hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao, isipo kuwa wale wapotofu walio kufuata. |
43. |
Na bila shaka Jahannamu ndipo pahali pao walipo ahidiwa wote. |
44. |
Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu walio tengewa. |
45. |
Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem. |
46. |
(Wataambiwa:) Ingieni kwa salama na amani. |
47. |
Na tutaondoa chuki iliyo kuwamo vifuani mwao, wawe ndugu juu ya viti vya enzi wameelekeana. |
48. |
Humo hayatawagusa machofu, wala hawatatolewa humo. |
49. |
Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. |
50. |
Na kwamba adhabu yangu ndio adhabu iliyo chungu! |
51. |
Na uwape khabari za wageni wa Ibrahim. |
52. |
Walipo ingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunakuogopeni. |
53. |
Wakasema: Usiogope. Sisi tunakubashiria kijana mwenye ujuzi. |
54. |
Akasema: Mnanibashiria nami uzee umenishika! Basi kwa njia gani mnanibashiria? |
55. |
Wakasema: Tunakubashiria kwa haki; basi usiwe miongoni mwa wanao kata tamaa. |
56. |
Akasema: Na nani anaye kata tamaa na rehema ya Mola wake Mlezi ila wale walio potea? |
57. |
Akasema: Hebu nini amri yenu, enyi wajumbe? |
58. |
Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu! |
59. |
Isipo kuwa walio mfuata Luut’i. Bila ya shaka sisi tutawaokoa hao wote. |
60. |
Ila mkewe. Tunakadiria huyo atakuwa miongoni watao bakia nyuma. |
61. |
Basi wale wajumbe walipo fika kwa Luut’i, |
62. |
Alisema (Luut’i): Hakika nyinyi ni watu msio juulikana. |
63. |
Wakasema: Bali sisi tumekuletea yale waliyo kuwa wakiyafanyia shaka. |
64. |
Na tumefika kwako kwa Haki, na hakika sisi tunasema kweli. |
65. |
Basi ondoka na ahli zako usiku ungalipo, nawe ufuate nyuma yao, wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma. Na mwende mnapo amrishwa. |
66. |
Na tukamfunulia hukumu hiyo, ya kwamba hata wa mwisho wao hao ikifika asubuhi atakuwa kesha katiliwa mbali. |
67. |
Na wakaja watu wa mji ule nao furahani. |
68. |
Akasema: Hakika hawa wageni wangu, basi msinifedheheshe. |
69. |
Na mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi. |
70. |
Wakasema: Sisi hatukukukataza usimkaribishe yeyote? |
71. |
Akasema: Hawa binti zangu, ikiwa nyinyi ni watendaji. |
72. |
Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao, wakihangaika ovyo. |
73. |
Ukelele ukawatwaa wakipambaukiwa. |
74. |
Na tukaigeuza nchi juu chini, na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo wa Motoni. |
75. |
Hakika katika hayo zipo ishara kwa waaguzi. |
76. |
Na miji hii ipo kwenye njia inayo pitiwa. |
77. |
Hakika katika hayo ipo ishara kwa Waumini. |
78. |
Na hakika watu wa Kichakani walikuwa wenye kudhulumu. |
79. |
Kwa hivyo tukawaadhibu. Na nchi mbili hizi ziko kwenye njia ilio wazi. |
80. |
Na bila ya shaka wakaazi wa Hijr waliwakanusha Mitume. |
81. |
Na tuliwapa ishara zetu, nao wakazipuuza. |
82. |
Nao walikuwa wakichonga majumba katika milima kwa amani. |
83. |
Basi ukelele ukawatwaa asubuhi. |
84. |
Hayakuwafaa waliyo kuwa wakiyachuma. |
85. |
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa ajili ya Haki. Na hakika Kiyama kitafika. Basi samehe msamaha mzuri. |
86. |
Hakika Mola wako Mlezi ndiye Muumbaji Mjuzi. |
87. |
Na tumekupa Aya saba zinazo somwa mara kwa mara, na Qur’ani Tukufu. |
88. |
Usivitumbulie macho yako vitu tulivyo waneemesha makundi fulani kati yao, wala usiwahuzunikie. Na wainamishie bawa lako (la huruma) Waumini. |
89. |
Na sema: Hakika mimi ni mwonyaji mwenye kubainisha. |
90. |
Kama hivyo tuliwateremshia walio gawa, |
91. |
Ambao wakaifanya Qur’ani vipande vipande. |
92. |
Basi Naapa kwa Mola wako Mlezi! Tutawahoji wote, |
93. |
Kwa waliyo kuwa wakiyatenda. |
94. |
Basi wewe yatangaze uliyo amrishwa, na jitenge na washirikina. |
95. |
Hakika Sisi tunatosha kukukinga na wanao kejeli. |
96. |
Hao wanao fanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yupo mungu mwingine. Basi, watakuja jua! |
97. |
Na Sisi tunajua kwa hakika kuwa wewe kifua chako kinaona dhiki kwa hayo wayasemayo. |
98. |
Basi mtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi, na uwe miongoni wanao msujudia. |
99. |
Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini. |